STORY-PENZI LA MSHUMAA
MTUNZI-MZIRAY F.M.
SEHEMU YA 8
Ilipoishia sehemu ya 7
“Sikilizeni
niwaambie,suala la dini haliwezi kupima upendo alionao mtu kwa mchumba
wake.Mnaweza mkaoana watu wa dini moja na msielewane.Au kama mnaona hiyo ni
mbaya mimi nipo tayari kubadilisha dini ili tuwe kitu kimoja.”
“Aaaaah!hapana
mwanangu huko umefika mbali sana.Endelea tu na hiyo ndoa yako ya mahakamani
haina neno.Mbona watu wanaoana kimila mabomani huko na ndoa zao zinakuwa vizuri
tu.Mwanangu Denis,sasa hivi sitaki kukubugdhi hata kidogo.Fanya maamuzi yako
mwenyewe.Kile unachoona ni sahihi na kitafurahisha moyo wako kifuate hicho
hicho.Sitaki baadae upate matatizo halafu utusingizie sisi.Mimi sina tena neno
na wewe,nakupa baraka zote katika ndoa yako na ninakutakia maisha mema.”Mzee
Mwamba aliamua kumuunga mkono mwanaye Denis baada ya jitihada zake za kutaka
kumzuia asimuoe Shaimaa kushindikana.
“Asante sana baba
yangu.Nashukuru mno kwa uelewa wako.”Denis aliinuka kwa shangwe na kumkumbatia
baba yake kwa furaha.
“Baba.”Brenda aliita
kwa unyonge.
“Nini!Unataka kuleta
umbea siyo?”Denis alimgeukia Brenda na kumpaka.
“Hebu huko,sijakuita
wewe!”Brenda alijibu kwa jeuri.
“Ehe!unasemaje?”Mzee
Mwamba aliuliza baada ya kuachiana na Denis.
“Yaani umekubali kaka
Denis amuoe huyo shangingi wake wa Kitanga?”
“Brenda
usinitafute,nani shangingi?Nitakubomoa sasa hivi.”Denis alikasirishwa sana na
maneno ya shombo toka kwa mdogo wake.
“Brenda funga huo
mdomo wako.Shenzi kabisa.Ujue huyu ni kaka yako hivyo unapaswa
kumheshimu.Pumbavu!Hayawani mkubwa wewe.”Mzee Mwamba alifoka kwa sauti ya
ukali.Brenda aliamua kukiacha kikao kile na kuingia zake chumbani.
“Mmmh!huyu ana
kisirani gani?”Bi Asma aliuliza kwa masikitiko baada ya binti yake kuondoka.
“Kwahiyo mama na wewe
umekubaliana na maamuzi ya baba?”Winfrida alimtupia mama yake swali hilo huku
akiwa na kimuhemuhe cha hali ya juu.
“Winfrida
jichunge,utamfuata Brenda sasa hivi.”Denis aliingilia kati.
“Mbona una kiherehere
sana.Kwanini mimi nimekuuliza wewe?”Winfrida alimzodoa kaka yake.
“Hivi mbona
mnanifuatilia sana au mnataka niwaoe nyie?”Denis alifoka.
“Heeeh!Denis maneno
gani hayo unayomwambia dada yako?Kwahiyo wasikuambie ukweli au?Mimi mwenyewe
sijakubaliana na nyie hata kidogo.Hivi baba Denis unaona ni sahihi kabisa Denis
amuoe huyo mwanamke aliyetaka kumtoa roho kwa mawazo?”Bi Asma hakukubaliana
hata chembe juu ya uamuzi alioutoa mume wake.Yeye pamoja na mabinti zake
hawakutaka hata kumsikia Shaimaa sembuse kumuona!
“Mwambie huyo
mama.”Winfrida alishadadia.
“We koma,tena ukome na
ukomae.Shika adabu yako,kiroboto mkubwa wewe.Kama unashindwa kuzungumza maneno
yenye busara mfuate mwenzio chumbani.Shenzi kabisa.Hivi ninyi wanawake huwa mna
akili za aina gani?”Mzee Mwamba hakutaka mzaha hata kidogo.
“Kwahiyo mimi na
wanangu tupo sawa?”Bi Asma hakufurahishwa na kauli ya mumewe.
“Sikuwa na maana hiyo
mke wangu.”Mzee Mwamba alijitetea.
“Hukuwa na maana
hiyo!Ulikuwa unamaanisha nini?Eti hizi akili za wanawake ni za aina gani?Ni za
aina hiyo hiyo unayoifahamu wewe.Kifupi ni kwamba simtaki huyo mchumba wa
Denis.Kama ameachana na Vivian amtafute mwanamke mwingine.”Mama yake Denis
alichafukwa kisawasawa.
“Mtafutie basi
wewe.”Mzee Mwamba aliropoka.
“Nimtafutie mimi!kwani
yeye ni bubu au kipofu?Halafu baba Denis mbona unanikosea heshima hapa mbele ya
watoto?Hivi ni picha gani tunayoitengeneza hapa?”Bi Asma aalizidi kufoka kwa
hasira.
“Iwe picha ya Kihindi
au ya Kizungu utajua mwenyewe.Mwanangu Denis,oa mwanamke yeyote unayemtaka mimi
nipo nyuma yako.”
“Aoe mwanamke yeyote
anayemtaka eeh!”
“Eeeh.”
“Wewe si ndiyo ulikuwa
mstari wa mbele kulipinga hili suala la Denis kumuoa huyo binti wa Kitanga?”Bi
Asma alimtazama mumewe na kumtwanga swali hilo kwa ukali.
“Nilikuwa namwonea tu
bure.Kwani mimi nililazimishwa kukuoa wewe?Si nilikuchagua mwenyewe.Wewe
ungelazimishwa ungekubali?”Bi Asma aliishiwa pozi baada ya mumewe kumhama na
kuhamia upande wa pili wa mwanaye.Denis alifurahi sana kuungwa mkono na baba
yake.Aliamini kuwa kama Mzee Mwamba yupo pamoja na yeye hata hao wengine
wakigoma haina shida.Ilimradi tu amepata baraka angalau za mzazi mmoja kila
kitu kitakwenda kama kilivyopangwa.Bi Asma alimshika bintiye mkono haoo
wakaingia zao chumbani na kuacha kikao kikitawaliwa na chips dume.
“Hivi kwanini mama
anapinga mimi kumuoa Shaimaa?”Denis aliuliza kwa unyonge.
“Achana na hayo
mambo.Hilo suala niachie mimi wala usiwe na wasiwasi.Najua nitazungumza naye
vipi mpaka akubaliane na hali halisi.We endelea na hiyo mipango yako,kila kitu
kitakuwa sawa.Vipi kuhusu suala la mahari,tunapeleka lini?Usije ukamchukua
binti wa watu bila wazazi wake kufahamu!”Kweli Mzee Mwamba alidhamiria kuwa
bega kwa bega na mwanaye.
“Kuhusu suala la
mahari baba nilishamalizana nalo muda mrefu.Niliongea na baadhi ya wazee ambao
ni marafiki zangu wakaenda ukweni kumalizana nao.Niliamua kufanya hivyo
kwasababu ninyi mlishaonesha kunitenga tangu mwanzoni kabisa.”Denis alizungumza
huku akiwa kayatupa macho yake pembeni kwa aibu kutokana na kitendo alichokifanya.
“Daah!mwanangu
Denis,kwanini ulichukua maamuzi ya haraka kiasi hicho?Umetudhalilisha sana sisi
wazazi wako.Sasa siku hiyo utatutambulishaje mbele ya wazee wenzetu?”Mzee
Mwamba alisikitishwa mno na maelezo ya Denis.
“Sasa baba unafikiri
mimi ningefanyaje?Ninyi ndiyo mna makosa na mnastahili kulaumiwa.Mmengekubali
tangu mwanzoni kuwa upande wangu haya yote yasingetokea.”Denis alimshushia baba
yake zigo za lawama.
“Utusamehe sana
mwanangu.Nilikuwa nang’ang’ania kitu ambacho kingepoteza furaha yako.Hiyo haina
shida,tutajua namna ya kuzungumza nao.Kwahiyo maandalizi ya harusi
yanaendeleaje?Nimesikia ukisema kuwa uhitaji kamati ya harusi sasa sijui hiyo
sherehe yako itakuaje?”Mzee Mwamba alitaka kujua kinachoendelea ilimradi
kufanikisha tukio hilo.
“Mimi sifanyi sherehe
ya kualika Tanzania nzima.Nafanya katafrija kadogo tu cha kishkaji ambayo
itaudhuriwa na watu wachache mno.Sitaki kuonekana mtu wa fahari sana ndiyo
maana nimeamua kufanya hivyo.”Denis alimfafanulia baba yake namna mambo
yalivyopangwa katika sherehe yake.
“Ni vizuri,mimi siwezi
kuingilia.Kwahiyo ni siku gani unatarajia kufunga hiyo ndoa yako?”Mzee Mwamba
alitaka kujua siku ya harusi hiyo.
“Nimepanga kufunga
ndoa siku ya Ijumaa katika mahakama ndogo ya Wilaya ya Mkuranga.”
“Haaa!kwahiyo umeamua
kufungia huko huko Mkuranga kwako unapokaa?”
“Ndiyo hivyo mzee,au
wewe unataka nifungie wapi?”
“Aaah!mimi sina
neno.Popote unapoona ni sahihi wewe kamilisha tu mambo yako.”
“Nashukuru sana baba
kwa kuniunga mkono.Ngoja nikakuchukulie mzigo kidogo kwaajili ya kununulia nguo
za sherehe hiyo.”
Denis alitoka nje na
kufungua mlango wa nyuma wa gari lake na kuibuka na brufkesi ndogo.Baada ya
hapo alifunga mlango wa gari na kuingia ndani ya nyumba yao. “Humo katika hilo
begi kuna kama milioni tano hivi.Mtatumia hizo pesa kununulia nguo na kama
hazitawatosha utanipigia simu niwaongezee.”
Denis alimkabidhi baba
yake zile pesa na kumpatia maelekezo ya matumuzi yake. “Nashukuru sana
mwanangu.Hizi pesa ni nyingi sana wala hazihitaji nyongeza yoyote ile.”Mzee alitoa
shukrani zake kwa mwanaye huyo aliyekuwa na utajiri wa hali ya juu.
“Usiogope kutumia pesa
zangu.Haya ndiyo matunda ya kuza dume la mbegu baba.Mkanunue nguo zinazoendana
na hadhi yenu.Sitaki kuwaona mkiwa mmevaa nguo za ajabu ajabu katika sherehe
yangu.Mtaenda na Brenda,yeye anafahamu maduka yenye nguo nzuri hapa mjini.Mimi
ningekuwa na nafasi ningewapeleka lakini nina mambo mengi mno ya kufanya.”Denis
alimtaka baba yake awe huru katika matumizi ya pesa zake.
“Usijali mwanangu,kila
kitu kitakwenda kama kilivyopangwa.”
“Baba ngoja sisi
tuondoke kwasababu kuna sehemu tunataka tupitie.Nafikiri naweza nikaja huku
kesho ama keshokutwa kuwajulia hali.”
“Haya mwanangu,Mungu
akutangulie katika mambo yako.Ila nasikitika mnaondoka kama mlivyokuja.Wadogo
zako bado hawajapika chai.Walipoamka tu wakakutana na ugeni wa Vivian ndiyo
tukaingia kikaangoni.Sasa hivi naona wameenda kujivundika ndani.”
“Aaah!usijali
mzee,sisi tupo kamili gado.Utatusaidia kumuaga mama pamoja na akina
Brenda.Nadhani sasa hivi bado wamechafukwa kutokana na hili lililotokea hapa.”
“Ha!ha!ha!ha!we nenda
baba mimi najua namna ya kuzungumza na mama yako naye akazungumza na
wanaye.Kila kitu kitakwenda sawa.”Mzee Mwamba alimtia mwanaye moyo na kumtakia
kila la heri katika kufanikisha mambo yake.
“Haya baba kwaheri.”
“Haya mwanangu,endelea
kuzitunza busara ulizokuwa nazo.”
“Ha!ha!ha!ha!nyie
wazee wetu ndiyo mna busara na hekima kushinda sisi.”Dick alipoaga,Mzee Mwamba
hakusita kumsifia kutokana na maneno yake ya busara aliyoyatoa katika kikao
kile.Walipofika nje Denis alimrukia rafiki yake kwa furaha nusura ambwage
chini.
“Yes!mambo si ndiyo
hayo.”
“Vipi Denis,mbona una
furaha namna hiyo?”Dick aliuliza kwa mshangao.
“Ujue wewe ndiyo
umesababisha baba abadilishe mawazo.”Denis aliongea huku akiongoza njia
kulifuata gari.
“Kivipi?”Dick
alipouliza swali hilo,Denis aliacha kufungua mlango wa gari na kumgeukia.
“Unaniuliza kivipi
tena?”
“Ndiyo.”
“We unadhani maneno
uliyoongea pale ni ya kitoto?Yaani umemkamata baba kisawasawa.Mimi namfahamu
Mzee Mwamba akishikilia jambo hata kama ni la kijinga hawezi kubadili msimamo
wake kirahisi namna hiyo.Lakini wewe umemuweza kweli kweli.Ujue sikuamini pale
baba alipoanza kuzungumza kwa upole baada ya wewe kutema cheche zako.Kwa jinsi
alivyokuwa anaongea nikajua hapa kwisha habari yake.”Denis alimsifia rafiki
yake kwa jinsi alivyozungumza maneno ya busara na kuulainisha moyo wa Mzee Mwamba ambapo aliamua kumwacha mwanaye
afanye maamuzi yake mwenyewe.
********
Itaendelea.....Nashukuru kwa ufuatiliaji wako wa hadithi hii naamini utajifunza mengi na utaburudika.Nakutakia siku njema na Mungu akubariki.
*******
Kw amaoni au ushauri napatiana kwa namba 0655089197/0766123623
2 comments
commentsKama kawaida...hadithi tamu za kumwaga ndani ya nyumba
ReplyKama kawaida...hadithi tamu za kumwaga ndani ya nyumba
Reply