STORY-PENZI LA MSHUMAA
MTUNZI-MZIRAY F.M.
SEHEMU YA 19
Ilipoishia sehemu ya 18
Tangu wazaliwe
hawajawahi kuingia katika hoteli ya kisasa kama hiyo na kupata msosi wa namna
ya kipekee.Muda wote walikuwa wanashangaashangaa kama vile wapo feri.Baada ya
kumaliza kupata kifungua kinywa Denis aliwaingiza wazee wale ndani ya gari lake
na kuanza safari ya kuelekea nyumbani kwao katika kata ya Chumbageni maeneo ya
Kisosora.Walipita kwenye mzunguko wa pale Kwaminchi na kunyoosha barabara
ambapo baada ya kuuvuka msikiti walikata kushoto na kuendelea na safari.
Sasa endelea....
Denis aliendelea
kuionea lami kwa kukanyaga mafuta mpaka alipoiacha barabara inayoelekea Ikulu
ndogo na kukata kulia.Hapo ndipo walipoingia rasmi mtaa wa Kisosora ambapo
kutokana na maelezo ya wazee wale Denis alifanikiwa kupaki gari mbele ya nyumba
yao.Nyumba ya familia hiyo ilikuwa ni ya udongo lakini ilipigwa plasta kwa nje
na kupakwa rangi.Juu iliezekwa kwa makuti na iliegemea upande mmoja kuashiria
kuwa muda wowote ingeweza kuanguka.
Denis alikaribishwa
stuli na kuketi pale barazani.Aliendelea kuyashibisha macho yake kwa kuangaza
huku na huko akiyasawiri vizuri mazingira yale.Watu wengi wa mtaa ule walitoka
na kujipitisha katika nyumba ile ili wajue ni nani aliyekuja na gari la kisasa
namna ile.Denis alizungumza mambo mengi sana na wale wazee ikiwemo kuwasaidia
kuboresha mazingira yao ya kuishi.Bi Zena na mumewe walifurahi sana na kuanza kujichekesha
kwa aibu baada ya kumkashfu mno kijana huyo.
“Tunashukuru sana
kijana wetu,Mungu akubariki na akuzidishie.”
“Asante sana baba kwa
ahadi yako.”
“Msijali wazee
wangu,haya ni mambo ya kawaida.Mimi ngoja niwaache kuna mambo yangu nataka
nikayafuatilie halafu jioni nitakwenda hospitali kumjulia hali Shaimaa sambamba
na kumpelekea chakula.”
“Hamna
tatizo,ubarikiwe sana baba.”
“Chukueni hiki kiasi
kidogo cha fedha kitawasaidia siku mbili tatu.Kesho nitakuja asubuhi kuwachukua
mkamwone mtoto wenu.Vile vile tutapanga namna ya kusafiri naye kuelekea
Dar-es-salaam.”
“Haya mwanangu,asante
sana baba.”Denis aliagana na wale wazee kisha akaenda shughuli zake
zilizompeleka Tanga.Angalau furaha ilirejea katika familia ya Mzee Kambi.Kitita
cha pesa walichoachiwa na Denis kiliwapagawisha mno.Siku hiyo hawakunywa pombe
ya mnazi,badala yake walienda kukata bia mpaka jioni.Walirejea nyumbani wakiwa
bwi!Waliwakuta wajukuu wao wakipiga miayo kwa njaa.
Bi Zena alitoa noti ya
shilingi kumi na kuwapa mabinti hao na kuwaambia wakale chochote
wanachokitaka.Wasichana hao walishangaa sana kwani haijawahi kutokea hata siku
moja wazee hao wakawapa pesa ya matumizi.Asubuhi wakati Denis alipokwenda
katika nyumba hiyo,wao walikuwa wamekwenda shuleni.
Siku iliyofuata
asubuhi na mapema Denis kama alivyoahidi aliwafuata Mzee Kambi na mkewe
wakaelekea Bombo hospitali ambayo ni hospitali ya mkoa wa Tanga.Walifanikiwa
kumwona Shaimaa ambaye bado hali yake haikuridhisha hata kidogo.
Walihuzunika sana
lakini ndani ya nyoyo zao kulijaa tumaini la kupona kwa binti yao baada ya
mipango yote ya safari ya kumhamihsia Muhimbili hospitali kukamilika.Wazazi wa
Shaimaa walimshangaza sana Denis kwa kumwambia kuwa yeye aondoke na Shaimaa
peke yake kwasababu wao watabaki kuwaangalia wale mabinti wanaosoma.Kilichomfanya
Denis ashangae zaidi ni namna wazee hao walivyomwamini haraka namna hiyo wakati
siku kadhaa zilizopita walikuwa wakali kama Mbogo aliyejeruhiwa.
“Yaani anayeumwa ni
binti yao halafu wananiambia niondoke naye mimi mwenyewe bila wao kuwepo!Mmmh!wana
lengo gani na mimi?Inamaana hawana ndugu yeyote atakayebaki na hao
watoto?Kwanza mbona wanaonekana ni mabinti wakubwa tu!”Denis aliamua kuzungumza
na Mzee Kambi ili angalau yeye aende naye halafu mkewe abaki kuangalia familia.
“Hapana kijana ni bora
mke wangu aende maana yeye ndiyo ataweza kumhudumia binti yake.Mimi nitabaki
nyumbani na hawa watoto wala hamna tatizo.”Mzee Kambi alijitoa kwenye mpango wa
kwenda Dar-es-salaam.
“Ni kweli kabisa hilo
ni wazo zuri.Mama,itabidi tusafiri wote.”Denis alilikubali wazo la Mzee Kambi
na kuona kuwa kuna umuhimu wa kwenda na mama mtu akamuuguze mwanaye.Ilibidi
atumie nguvu ya ziada kumshawishi mama huyo akubali kwenda kumhudumia mwanaye
atakapokuwa hospitali.Sababu kubwa iliyokuwa inawafanya wazee hao wawe wagumu kwenda
Dar-es-salaam ni kuhofia kuzikosa starehe wanazozifanya pale Tanga.
Ni jambo la kushangaza
sana kwa wazazi kukwepa kwenda kuuguza binti yao eti kisa starehe zisizokuwa na
misingi yoyote na kumwachia mzigo wote mtu ambaye hausiki kabisa na familia ile.Baada
ya Denis kusisitiza sana ilibidi Bi Zena akubali kwa shingo upande.Walipotoka
pale Bombo hospitali walielekea kituo cha polisi Raskazoni kufuata vitambulisho
vya Denis.Wazazi wa Shaimaa waliomba kesi hiyo ifutwe baada ya Denis kuonesha
moyo wa kuwasaidia kwa hali na mali.
Hata hivyo pesa za
kuifuta kesi hiyo alizotoa Denis mwenyewe kwa kuwa alikuwa anataka vitambulisho
vyake.Baada ya kutoa fedha alipewa vitu vyake sambamba na kitambulisho cha Dick
alichokiacha kama mtoa dhamana wa Denis.Walipotoka hapo walipitia hotelini na
kupata chakula kisha Denis akawarudisha wazee hao nyumbani kwao na kumwambia Bi
Zena ajiandae kwa safari ya siku inayofuata.Denis hakutaka kumwambia mtu yeyote
kuwa anarejea Dar-es-salaam kesho yake.Aliamua kufanya hivyo ili kuwashtukiza
wazazi wake pindi atakapokwenda kuwajulia hali.
Palipopambazuka tu
Denis alienda kukabidhi funguo wa chumba pale mapokezi na kuwashukuru kwa
huduma nzuri waliompatia.Yule dada wa mapokezi naye hakusita kumshukuru kwa
niaba ya uongozi wa hoteli na kumkaribisha kwa mara nyingine tena.Denis
aliingia ndani ya gari lake na kuelekea Kisosora kumchukua Bi Zena.
Alipofika alipokelewa
na Mzee Kambi na kumwambia kuwa mkewe yupo chumbani anajiandaa.Waliendelea na
maongezi pale barazani huku muda ukizidi kuyoyoma bila Bi Zena kutokea.Denis
alishangazwa sana na hali ile mpaka akadhani pengine mama huyo ameghairi
safari.
“Mzee mbona mkeo
hatoki kuna tatizo gani?”Baada ya uvumilivu kumshinda,Denis aliamua kuuliza
kulikoni.
“Wewe mama
Shaimaa.”Mzee Kambi aliita kwa sauti ya juu.
“Abee mume wangu.”
“Unafanya nini huko
ndani mwaka mzima?Muda haukusubiri wewe,unamchelewesha kijana wa watu hapa.”
“Nakuja.”
“Haya fanya
haraka.Usijali kijana,anakuja sasa hivi.”Dakika ishirini zilipita tena bila Bi
Zena kutokea.
“Mzee vipi,mbona
hatoki tena?”Denis alihoji kwa hasira.
“We mama Shaimaa!”
“Ndiyo nakuja
jamani.Hee!kwahiyo nisijitengeneze?Mwanamke urembo babu wewe!”
“Haya mimi
sikuwezi.”Mzee Kambi aliongea kinyonge.
Mama huyo alipotoka
nje hakutamanika.Jini siyo jini,msukule siyo msukule.Yaani kifupi ni kwamba
hakueleweka kama ni msichana au mama mtu mzima.Alikuwa amejipara si
mchezo.Alipaka rangi za aina tofauti tofauti katika macho yake.Mdomo aliukoleza
kwa rangi nyekundu huku uso wake akiumiminia poda kopo zima.Vile vile
alijimwagia urembo mwingine uliokuwa unametameta na kuufanya uso wake kuonekana
kama ukumbi wa disko.
Kichwani alijivika
manywele ya bandia yaliyozidi kuupoteza uhalisia wake.Pia alikuwa amejichora kwa
ina mwili mzima.Muonekano wake ulimkera sana Denis lakini alishindwa kumwambia
ukweli mama huyo.Aliishia kumwangalia kwa hasira huku akimezea maneno yake
ndani kwa ndani ili asionekane mtu aliyekosa heshima mbele ya watu wazima.
“Shoga,naona
umeshatokelezea,wapi hiyo?”Wakati mama huyo akiwa anapeleka begi lake kwenye
gari mara mashosti zake wawili wakatokea kufuata ubuyu.
“Naelekea zangu Dar
kula maisha.”Bi Zena alijibu kwa mbwembwe.
“Unaenda Dar
mwenzetu!”
“Sasa je!”
“Kwa nani?”
“Si mnamuona huyo
dogodogo wangu hapo?”
“Namuona,halafu
inaelekea mambo safi si mchezo.”
“Mmmh!shoga,huyo ni
bonge moja la tajiri.Kama nisipompata mimi basi lazima mwanangu Shaimaa
amnase.”Bi Zena alijitamba.
“Loo!inamaana bado
hujamuonjesha tu?”
“Bado shoga,ndiyo
kwanza nimeanza naye mazoea juzi juzi tu.Sasa hivi tunamuhamishia Shaimaa
Muhimbili na huyu ndiyo analipa kila kitu.”
“Basi nikuambie kitu
shosti?”
“Nipe ubuyu huo.”
“Huyu muache Shaimaa
ndiyo atamnasa vizuri.”
“Sawa,lakini siku hizi
mwanangu anajifanya kaacha mambo hayo eti yupo bize anawatunza watoto wake kwa
kuuza Uono.”
“Shoga,itabidi
tumkalishe chini tumwambie.Hii ni bahati na siku zote huwa haiji mara
mbili.Yeye ashangae shange ataishia kuuza Uono wenzake wanatembelea magari.”
*******
Je nini kitaendelea?Usikose sehemu ijayo ya simulizi yetu iliyojaa visa na mikasa ya kusisimua.Naamini unaendelea kujifunza siku hadi siku na pia unaburudika vya kutosha.Nakutakia siku njema na Mungu akubariki sana.
*******
Kwa maoni au ushauri napatikana kwa namba 0655089197/0766123623