STORY-PENZI LA MSHUMAA
MTUNZI-MZIRAY F.M
SEHEMU YA 12
Ilipoishia sehemu ya 11
“Ungekuwa hujamgonga
wewe ungenipa fedha ili tuyamalize?Kwanini unataka kumkimbia binti wa watu
wakati wewe ndiyo umemvunja miguu?Tumeshakumbana sana na kesi nyingi za namna
hii ndiyo maana sasa hivi hatutaki mchezo hata kidogo.Kuna watu wamekaa humu
hospitali huu ni mwaka wa pili kwa kukosa msaada baada ya kukimbiwa na ndugu
zao au watu kama ninyi mliowasababbishia matatizo.Sasa hivi tumekuwa macho
hatutaki suala hili lijirudie tena.”
Sasa endelea.......
Yule dokta alizungumza
kwa hisia kali akilalamikia vitendo vya watu kuwasusia wagonjwa wao pale
hospitali bila msaada wowote.Aliamini kuwa Denis ni mmoja wa watu kama hao
baada ya yule binti kukiri kuwa Denis ndiyo kamsababishia ajali.
“Ila dokta mnanione
tu,mimi sihusiki na ajali hiyo.”Denis alizidi kujitetea.
“Hayo masuala utakuja
kuwaleza polisi watakapofika hapa.”Dokta hakutaka malumbano na Denis badala
yake alimwambia kuwa awasubiri polisi wafike ndipo ajitetee.Denis hakuwa na
jinsi,aliamua kudondosha shingo yake chini kwa masikitiko.Baada ya dakika tano
polisi wakiwa na silaha mkononi walifika pale hospitali na kueleza kuwa
walipigiwa simu na mmoja wa madaktari wa pale.Wakati Denis akiwa kajiinamia
chini mara simu ya yule dokta aliyekuwa naye ikaita.
“Hello!habari ni nzuri
tu.”dokta alipokea simu na kuanza kuongea. “Yaa!mimi ndiyo
niliwapigia,waelekeze katika chumba changu.Haya okay,nashukuru sana.”Denis
aliinua uso wake na kumtazama yule dokta kwa hasira.Kabla hajafanya kitu
chochote mara mlango wa kile chumba ukagongwa mara mbili.
“Ngo!ngo!”
“Pita tu mlango upo
wazi.”Dokta alitoa ruhusa ya aliyekuwa anagonga kuingia ndani ya chumba.
“Oooh!maafande
karibuni sana.Kijana mwenyewe anayeleta mushkeli kidogo ndiyo huyu
hapa.Amesababisha ajali halafu anataka kukimbia.Amemgonga binti mmoja ambaye
kwa sasa yupo hodini na kumvunja miguu yote.Sasa anataka kumtelekeza halafu
yeye ayoyome zake.Mambo haya yameshatokea sana hapa hospitali na ndiyo maana
safari hii tukawa makini mno.”Dokta aliwaeleza wale askari sababu iliyomfanya
awaite pale
“Dokta nimeshakwambia
huyo binti ni muongo.”
“Funga mdomo
wako.Pumbavu!”Askari mmoja alimnyamazisha Denis kwa sauti ya ukali.
“Nyie ndiyo mnaua watu
halafu mnawakimbia siyo?Dokta,tunaweza kuzungumza na huyo binti ili athibitishe
hili suala?”Askari mwingine alidakia na kumuuliza dokta kama kuna uwezekano wa
kumsikia binti mwenyewe akizungumza.
“Hakuna tatizo
tunaweza kwenda kumuona.”Dokta aliwachukua wale askari wakiwa na Denis kuelekea
katika kile chumba alicholazwa yule binti.Baada ya kufika askari mmoja alianza
kumhoji taratibu.
“Binti unaitwa nani?”
“Naitwa Shaimaa.”Yule
msichana alijibu kwa sauti ya chini.
“Pole sana binti kwa
yaliyokukuta.”
“Asante afande.”
“Unamfahamu huyu
kijana?”Denis alisogezwa karibu na yule binti aliyejitambulisha kwa jina la Shaimaa.
“Ndiyo namfahamu.”
“Tumepigiwa simu na
kuambiwa kuwa anataka kutoroka.Sasa tumekuja hapa ili kupata maelezo yako juu
ya ajali iliyotokea.”Maelezo aliyoyatoa Shaimaa hayakutofautiniana na yale
maelezo aliyowapa wale madaktari mwanzoni.Alizidi kushikilia msimamo wake
kwamba Denis ndiyo aliyemgonga kwa gari lake la kifahari.Kauli hiyo aliitoa
huku akiwa anamwaga machozi kwa kumlaumu kijana huyo kuwa amempa ulemavu wa
maisha.
“Huyu binti katumwa
nini?We dada,una uhakika kuwa mimi ndiyo nimekugonga?Muulizeni aliniona vipi
wakati yeye alikuwa kwenye pikipiki.”Denis alishindwa kuelewa ni jinamizi gani
limekumba ndani ya jiji hilo.
“Kelele wewe.”Afande
mmoja alimfokea Denis.
“Siyo suala la
kelele.Dokta,hebu mpimeni huyo msichana pengine amechanganyikiwa.”
“Mimi
sijachanganyikiwa wala nini.Wewe ndiyo umenigonga kwa gari lako.Nilikushuhudia
kabisa kwa macho yangu ukiniletea gari miguuni wakati nilipokuwa navuka
barabara.Watu walikusihi upunguze mwendo lakini hukutaka kusikia.Baada ya
kunigonga ukajidai eti unanisaidia kinafki ili raia wenye hasira kali
wasikushambulie.Umefika hapa unataka kunikimbia ilihali umeshaniharibia maisha
yangu.”Shaimaa aliendelea kukazia maelezo yake.
“Haaa!hata aibu
huna!Mungu wangu!wema wangu ndiyo umeniponza.Kwahiyo bora ningekuacha pale pale
ufe kuliko huu usamaria nilioufanya?”Moyo wa Denis ulikunjwa ndita kwa
hasira.Alitamani amrukie Shaimaa pale alipolala na kummaliza lakini aliona
atajizidishia matatizo zaidi.Sekunde kadhaa baada ya Denis kumaliza kuongea
mara mlango wa chumba kile ukafunguliwa
akaingia nesi akiwa na watu wanne.Kulikuwa na baba mmoja wa makamo kidogo na
mama mmoja aliyeeonekana kama mkewe.Vile vile walikuwa na mabinti wawili
waliokwishavunja ungo.
“Oooh!mwanangu Shaimaa
pole sana kwa yaliyokukuta.Uuuwiii!mwanangu umeshakuwa kilema.Eeeh Mungu
kwanini umeiandama familia yetu kiasi hiki?”Yule mama alianza kupiga mayowe
baada tu ya kumwona Shaimaa akiwa kalala juu ya kitanda cha wagonjwa.
“Mamaaa!mamaaaaa!mwanao
nakufa!Baba!baba mtoto wako nimeshakuwa mlemavu!Nitaishije mimi jamani
mie.”Shaimaa naye alipowaona wazazi wake alianza kupiga kelele za uchungu.
Daktari pamoja na nesi
waliwasihi wapunguze kelele kwani mgonjwa anaweza akazidiwa kutokana na uchungu
atakaoupata.Mama alimfuta mwanaye machozi na kumbusu kwenye paji la uso
wake.Baba alisalimiana na watu wote waliokuwa ndani ya chumba kile.Pia mama
alifanya kama mume wake alivyofanya na wale wasichana nao wakafuata.
Wakati Denis alipokuwa
kwa daktari,Shaimaa alimpatia nesi namba za wazazi wake na kuwasiliana nao ili
kuwaeleza hali iliyompata binti yao.Baada ya nesi kuwapigia wazee hao na kuwapa
habari hizo,walifunga safari wakiwa roho juu juu mpaka Bombo hospitali ambapo
walielekezwa chumba alicholazwa Shaimaa na kwenda kumtazama.
“Kwahiyo maafisa
mmefanikiwa kumkamata huyo kijana aliyemgonga binti yangu?”Maelezo aliyoyatoa
yule nesi wakati alipowasiliana na wazazi wa Shaimaa ndiyo yale yale
aliyowaleleza binti huyo kuwa aligongwa na gari wala siyo pikipiki.Jambo hilo
lilimfanya Mzee Kambi ambaye ni baba yake Shaimaa kuwahoji wale polisi
waliokuwepo ndani ya hodi ile.
“Usiwe na wasiwasi
mzee,kijana mwenyewe tunaye hapa.”Askari mmoja alijibu kwa kujiamini.
“Yupo wapi?Au ndiyo
huyu hapa?”Mzee Kambi aligeuka na kumtazama Denis aliyekuwa ameshikilia funguo
za gari lake huku nguo zake zikiwa zimetapakaa damu.
“Haswaaa,ndiyo
huyu.”Askari mmoja alimthibitishia mzee huyo kuwa aliyekuwa anamtazama ndiyo
kijana aliyemgonga binti yake.
“Kijana unataka
kuniulia mwanangu,shenzi kabisa!Zaa wako umtoe roho.”Mze Kambi aliinuka na
kutaka kumvamia Denis kama tingatinga lakini askari waliweza kumdhibiti
asifanye kitendo hicho.Alitulizwa na kuambiwa kuwa asiwe na shaka kila kitu
kitakuwa sawa kabisa kwasababu mtuhumiwa yupo mikononi mwao.Japokuwa mzee huyo
alionekana mwenye afya mgogoro lakini ni mshari balaa!
“Usipaniki mzee,huyu
kijana tayari yupo katika mikono ya chombo cha dola hivyo acha sheria ichukue
mkondo wake.”Denis alimkata Shaimaa jicho la hasira kutokana na kumsingizia
kosa ambalo hakulitenda yeye.
“Unamwangalia nini
mwanangu?Ulitaka kumuua halafu sasa hivi unamwangalia kwa macho yako ya
kichawi!Mwanga mkubwa wewe.”Mama yake Shaimaa anayejulikana kwa jina la Bi Zena
alikasirishwa mno na kitendo cha Denis kumwangalia binti yake.Hapakuwa na
jinsi,Denis alifungwa pingu na kutolewa nje ya jengo lile.
Waliingia ndani ya
gari lake ambapo askari mmoja aliendesha mpaka kituoni maeneo ya
Raskazoni.Walipofika kituoni Denis aliingizwa chumba cha mahojiano na kuanza
kuhojiwa. “Kijana kwanini umegonga mtu halafu unataka kukimbia?”
“Afande naongea ukweli
kabisa mimi sijamgonga yule binti.Alipata ajali ya pikipiki pale kwa Kwaminchi
karibu na reli.”Denis alijaribu kujitetea.
“Nyamaza!unadhani sisi
ni watoto wadogo au?Huu ndio mchezo wenu wa kila siku.Mkishakuwa na magari ya
mikopo basi mnajiona ndiyo mmefika mnatawala barabara nzima.Hivi kwanza una
leseni kweli wewe?”
“Ndiyo,ninayo.”Denis
alijibu kinyonge.
“Ipo wapi?”
“Kwenye gari.”
“Twende
ukaichukue.”Denis alitolewa nje akiwa na pingu zake mkononi.Walielekea moja kwa
moja mpaka kwenye gari na kutoa leseni katika begi lake.
********
Itaendelea....Nashukuru kwa ufuatiliaji wako wa hadithi hii...Nakutakia siku njema na Mungu akubariki sana.
*********
Kwa maoni au ushauri napatikana kwa namba 0655089197/0766123623