STORY-PENZI LA MSHUMAA
MTUNZI-MZIRAY F.M.
SEHEMU YA 18
Ilipoishia sehemu ya 17
“Tena mtihani mzito
kweli kweli kwa wazazi wa huyu binti siyo kwako.Umewatia dosari ya
maisha.Wameniambia kuwa huyo binti ndiyo tegemeo lao pale nyumbani.Wao hawana
shughuli yoyote ya kuwaingizia kipato.Wamesema kuwa Shaimaa ndiyo alikuwa
anatoka na kwenda kubangaizabangaiza mitaani na kuwaletea chochote kitu.Tangu
mtoto wao apate ajali hawajaingiza chochote mdomoni na ukizingatia wanaishi na
mabinti wadogo wawili wanaosoma.Wamekilaumu sana kitendo ulichomfanyia binti
yao ambacho kimeathiri familia nzima.Kwahiyo kijana tambua kuwa laana ya wazee
hao itakusumbua maisha yako yote.”
Sasa tiririka nayo......
Dokta alimweleza Denis
mambo ambayo yaliuumiza sana moyo wake.Japokuwa yeye hakuhusika kwa chochote
kile juu ya ajali ya Shaimaa lakini hali ya familia yake ilimpa sononeko la
moyo.Kitendo cha kusikia kuwa Shaimaa ndiyo alikuwa mhimili wa familia yao
kilimsikitisha sana.
Shaimaa alikuwa
anafanya biashara ya kuuza dagaa wabichi wanaojulikana kwa jina maarufu la Uono
huko mkoani Tanga.Mtaji wake ulikuwa ni mdogo sana hivyo hakuwa na biashara
kubwa ya kuridhusha.
Alikuwa anapitisha
nyumba hadi nyumba kwa kutumia baiskeli yake aliyoifunga kikapu cha dagaa kwa
nyuma.Faida iliyopatikana ilikuwa ni kidogo mno ambayo ilitumika kununulia mlo
wa siku.
Wazazi wake hawakuwa
na kazi yoyote ile ya kuwaingiza kipato.Baba yake Shaimaa,Mzee Kambi muda wote
alishinda kwenye vilabu vya pombe ya mnazi.Vile vile alikuwa ni maarufu sana
kwa mchezo wa bao ambapo aliwanyanyasa wazee wenzake kila kukicha.Wakati
mwingine alipokosa pesa ya kununulia pombe aliingia chumbani kwa binti yake na
kumwibia fedha zake za biashara.Akitoka asubuhi anarejea saa 6 usiku ambapo
analeta vurugu nyumba nzima.
Mke wa mzee huyo,Bi
Zena,naye alikuwa hajatulia hata kidogo.Muda wote alijipamba kwa kujichora ina
mwili mzima sambamba na kutinda nyusi zake na kutengeneza kope.Akishapendeza
anaelekea kwa mashangingi wenzake ambapo walipiga domo kuanzia asubuhi hadi
jioni.Wakishatoka hapo wanatafuta sehemu yenye kigodoro na kwenda kukata mauno
mpaka asubuhi.Naye suala la kulewa ilikuwa ni kawaida yake tena kushinda hata
mumewe.
Pombe hizo alikuwa
ananunuliwa na vijana wadogo ambao ni sawa na watoto wake na mwisho wa siku
wanaenda kulipana gesti.Mwanzoni Shaimaa naye alikuwa na tabia kama ya mama
yake lakini baada ya kudungwa mimba mara mbili akapata akili.Aliamua kupambana
kwaajili ya wanaye baada ya kususiwa na baba zao.Alijaribu kila njia kuwashauri
wazazi wake ili waachane na tabia hizo lakini jitihada zake zote ziligonga
mwamba.
Wazee hao hawakuwa na
sehemu nyingine yoyote ya kupata chakula zaidi ya pale nyumbani.Hivyo
basi,Shaimaa ndiyo alikuwa tegemeo lao kwa kila kitu.Hawakubahatika kupata
mtoto mwingine zaidi ya binti huyo katika maisha yao ya ndoa.
Ilifikia hatua wazee
hao wakawa na madeni kila kona baada ya kukopa pesa za pombe.Binti huyo ndiye
aliyekuwa na jukumu la kupunguza madeni hayo siku ambazo biashara zake
zilikwenda vizuri.Kwasababu binti huyo alikuwa maarufu sana pale mtaani kwao
kutokana na tabia ya familia yake,ilimuwiya vigumu mno kuanzisha biashara hiyo
ya dagaa aina ya Uono kwa mara ya kwanza.Vijana wenzake hasa wasichana
walimcheka sana mpaka akatamani kuiacha.
Lakini kila alipowatazama
watoto wake aliwaonea huruma hivyo ikamlazimu kupambana.Hakuona umuhimu tena wa
kuugawa mwili wake ovyo kwa wanaume ili wamapatie msaada kama alivyokuwa
anafanya kipindi cha nyuma akiwa na marafiki zake.Kila siku alfajiri Shaimaa
alidamka na kuelekea baharini kununua hao dagaa wabichi toka kwa wavuvi na
kuanza kuwapitisha mitaani.
Biashara hiyo ndiyo
iliyowawezesha wanafamilia hao kuingiza mkono kinywani na kuelekea
msalani.Hivyo basi,tangu Shaimaa alipopata ajali hali imekuwa siyo hali pale
nyumbani.Hata kupata mlo wa siku imekuwa ni tabu.Si baba wala mama aliyekuwa na
kazi ya kufanya.Walikuwa na madeni kila mtaa ndiyo maana walishindwa hata
kwenda kukopa unga angalau wapike hata uji wa tangawizi.Hali hiyo ndiyo
iliyowafanya wazee hao wamlaani Denis wakiamini kuwa yeye ndiyo aliyeleta
matatizo katika familia yao baada ya tegemeo lao kuishia kulala tu kitandani
bila matumaini yoyote.
Denis aliinamisha
kichwa chake chini na kushusha pumzi ndefu baada ya daktari kumweleza hali
halisi ya Shaimaa ilivyokuwa mbaya pamoja na hali ya wazazi wake.Aliinua tena
uso wake na kumtazama dokta usoni kisha akamtwanga swali.
“Naweza kumwona
mgonjwa?”
“Hapana,kwa sasa hivi
yupo katika chuba maalumu cha upasuaji ambapo madaktari walikuwa wanashughulika
naye bila matumaini.”Dokta alimweleza Denis kuwa hatoweza kumuona Shaimaa kwa
wakati ule.
“Kwahiyo gharama za
matibabu mpaka sasa hivi ni kiasi gani?”Denis alipigiwa mahesabu ya gharama
zote alizotumia Shaimaa katika matibabu na baada ya kupewa alitoa pochi yake na
kuzilipa pesa zote.Alipewa risiti yake kisha akataka kujua utaratibu wa
kumwamishia mgonjwa Muhimbili.
“Sisi tutakuandikia
hapa,tutakupa kadi pamoja na faili lake kisha utakwenda pale Muhimbili kwenye
kitengo cha mifupa.Ukishafika hapo madaktari watamwangalia mgonjwa na huduma
itaanza mara moja.”
“Kwahiyo kuna
uwezekano wa kuondoka naye lini?”
“Nafikiri keshokutwa
kwasababu leo ndiyo kapata huo upasuaji mwingine mdogo.Nadhani siku ya kesho
ataitumia kwa mapumziko halafu hiyo keshokutwa muondoke naye.”
“Nashukuru sana dokta,ngoja
nikajaribu kuzungumza na wazazi wa binti huyo maana wamenishupalia mno.”
“Usijali,ngoja tuende
wote nikawaeleweshe.”
“Nitashukuru
sana.”Dokta na Denis walitoka nje ya chumba kile kwa lengo la kwenda kuzungumza
na wazazi wa Shaimaa waliokuwa wamefura kwa hasira.Moyo wa Denis ulishafunguka
na kukubali kuubeba mzigo usiomhusu.Maelezo ya yule dokta kuhusu hali ya
familia ya binti huyo jinsi ilivyo iliuchoma moyo wake na kuamua kutoa msaada
kwa roho nyeupe kabisa.
“Dokta vipi hali ya
binti yetu?”Walipofika nje,Bi Zena aliinuka kwa shauku ya kutaka kujua hali ya
mwanaye.
“Hali ya mtoto wenu
siyo nzuri sana lakini kuna tumaini la………….”
“We nyang’au unaona
sasa ulivyoingiza balaa katika familia yetu?Umeshamuua mtoto wetu na hatujui
tutaishije tena pale nyumbani.Yeye ndiyo kila kitu kwetu.Kama akifa
nakuhakikishia hata wewe hutochukua raundi lazima umfuate.”Mzee Kambi hakutaka
hata kusikiliza maelezo ya daktari.Alimrukia Denis kwa maneno na vitisho vya
hali ya juu.
“Sikiliza kwanza mzee
wangu,hebu punguzeni munkari ili tuelewane.”Dokta alijaribu kumpoza Mzee Kambi.
“Apunguze munkari wa
nini?Au kwa kuwa siyo mtoto wako aliyepata matatizo?Nakuambia hivi
kijana,mwanangu akifa lazima umtafune nyama.Shaimaa ndiyo alikuwa tegemezi letu
halafu wewe kwa makusudi ukaamua kumvunja miguu yake.Sijui umetumwa we
mwanga!”Bi Zena naye hakutaka kutulia.Alifunga kibwebwe kwaajili ya kumpasha
Denis.Nyoyo zao zilijaa jazba ya hali ya juu
kutokana na majanga aliyoyapata binti yao ambapo waliamini kuwa Denis
ndiyo chanzo cha yote hayo.
“Nadhani kila mmoja
akiwa na jazba hatutaweza kutatua jambo lolote hapa.Chamsingi ni kuzipunguza
hasira zetu ili tujue tunaokoaje maisha ya Shaimaa.”Baada ya wazee wale kupiga
sana kelele mwishowe wakachoka na kuamua kutulia.Denis aliumia sana moyoni kwa
kupewa shutuma zisizomhusu.Kuna wakati aliwaza kusitisha kabisa msaada wake na
kulipeleka shauri hilo mahakamani ambapo aliamini kuwa huko haki ingetendeka.
Lakini alipokumbuka
maelezo ya dokta kuwa Shaimaa ndiyo alikuwa mhimili wa familia yao moyo
ukamsuta.Aliamua kujikaza kiume ili amuokoe binadamu mwenzake.Hakutaka kuutumia
utajiri wake vibaya badala yake alipenda kuwasaidia wasiokuwa nacho lakini si
kwa kusingiziwa kosa ambalo siyo lake.
“Nimezungumza na
kijana hapa amekubali kulipa fedha za kumhamishia binti yenu Muhimbili jijini
Dar-es-salaama akapate matibabu ya kina zaidi.Msiwe na wasiwasi Shaimaa lazima
apone.”Dokta aliwaleza hayo wazazi wa Shaimaa kwa sauti ya upole.
“Sina hakika kama
mwanangu atapona.Si ulisema anaweza akakatwa miguu yake?”Bi Zena alizungumza
kwa unyonge.Hakuwa na imani kama mwanaye atapona tena na kurudi katika hali
yake ya kawaida.
“Kwa kuwa anakwenda
Dar-es-salaam kwenye hospitali ya taifa hakuna shaka kabisa lazima atakuwa
vizuri.La muhimu ni kumwomba Mwenyezi Mungu atie baraka zake na kila kitu
kitakuwa salama salimini.”
“Sawa dokta
tumekuelewa lakini tambua kuwa Shaimaa ndiyo alikuwa tegemeo letu pale
nyumbani.Sasa hivi hatuna msaada wowote ule.Kama tulivyokuambia leo ni siku ya
tatu hatujala chochote zadi ya kunywa tu
maji.”Bi Zena alianza kueleza matatizo ya familia yake kwa uchungu.
“Hilo halina tatizo
mama.Mimi nitabeba jukumu la kuwahudumia mpaka pale mtoto wenu
atakapopona.Kwahiyo kwa hilo wala msijali kabisa,tupo pamoja.”Na maneno yote ya
kejeli na lawama alizopewa lakini Denis bado alikuwa na moyo wa kuwasaidia
wanafamilia wale.
“Mmmmh!kwa jinsi
navyokuona na roho mbaya yako utatusaidia kweli?”Mzee Kambi bado alijifanya
jeuri.Msaada aliuhitaji lakini hakuacha kuendelea kutoa lawama zake kwa
Denis.Uchungu uliendelea kuutafuta moyo wa Denis lakini alijikaza kiume.Denis
aliwachukua wazee hao na kuwapeleka Dophin hoteli na kuwanunuliwa kufungua
kinywa cha nguvu.Mzee Kambi na mkewe hawakuamini kilichotokea.
Tangu wazaliwe
hawajawahi kuingia katika hoteli ya kisasa kama hiyo na kupata msosi wa namna
ya kipekee.Muda wote walikuwa wanashangaashangaa kama vile wapo feri.Baada ya
kumaliza kupata kifungua kinywa Denis aliwaingiza wazee wale ndani ya gari lake
na kuanza safari ya kuelekea nyumbani kwao katika kata ya Chumbageni maeneo ya
Kisosora.Walipita kwenye mzunguko wa pale Kwaminchi na kunyoosha barabara
ambapo baada ya kuuvuka msikiti walikata kushoto na kuendelea na safari.
********
Je nini kitafuata?Usikose mwendelezo wa simulizi hii iliyojaa visa na mikasa ya kusisismua siku ya Jumatano.Natumaini unaburudika na unaendelea kujifunza mengi kila iitwapo leo.Nakutakia siku njema na Mungu akubariki sana.
******
Kwa maoni au ushauri napatikana kwa namba 06550891987/0766123623