STORY-PENZI LA MSHUMAA MTUNZI-MZIRAY F.M. SEHEMU YA 22 Unknown 22:46 Unknown STORY-PENZI LA MSHUMAA MTUNZI-MZIRAY F.M. SEHEMU YA 22 Ilipoishia sehemu ya 21 Denis alishusha pumzi ndefu baada ya kumaliza meseji hiyo yenye ujumbe mzito toka kwa mchumba wake Vivian.Mawazo kibao yalivurugana ndani ya ubongo wake na kumfanya ahisi joto lililopitiliza ukizingatia ndani ya gari kulikuwa na Air Condition(AC).Denis alimpenda sana Vivian na wala hakuwa tayari kumpoteza msichana huyo kirahisi namna hiyo.Alitafuta namba yake na kubofya kitufe cha kupigia kisha akaiweka simu sikioni.Simu iliita ikakata,akaamua kupiga tena.Safari hii iliita wee kisha ikakatwa.Alipopiga tena ikawa haipatikani.Aliupiga usukani wa gari kwa mikono yake mara tatu kwa hasira halafu akaukumbatia. Sasa tiririka nayo....... “Huyu msichana ana tatizo gani?Mbona hataki kuwa mwelewa jamani!Mimi nimeshamwambia Shaimaa namsaidia tu wala siyo mpenzi wangu.Yeye anang’ang’ania eti nina mahusiano naye tena pamoja na mama yake!Hivi inaingia akilini kweli hiyo?”Denis aliendelea kutawaliwa na mawazo kedekede juu ya hali ya mapenzi yake iliyoanza kwenda mrama.Alishindwa kuelewa ni kwanini Vivian ameshindwa kumwamini mpaka akawa anamshutumu kwa kitu ambacho wala hakuwahi kukifikiria katika maisha yake. “Denis!Denis!We Denis.”Denis alikurupuka baada ya kusikia sauti ya Dick ikimwita. “We vipi?Hoteli yenyewe si ndiyo hii hapa au?Mbona unaendelea kung’ang’ania humo ndani?”Dolan aliyekuwa upande wa dirisha la kushoto la gari alianza kumtwanga Denis maswali hayo mfululizo. “Denis una matatizo gani mbona kama vile haupo sawa?”Dick aliyekuwa upande wa kulia akichungulia,naye akaamua kumtwanga rafiki yake swali hilo.Walipofika katika hoteli hiyo walipaki gari lao kisha wakashuka na kumsubiria Denis ambaye alikaa muda mrefu ndani ya gari lake.Kuona hivyo ndiyo wakaamua kumfuata na kumuuliza kulikoni.Denis alishuka kwenye gari akiwa mnyonge sana kiasi cha kuwashangaza wenzake. “Kwani kuna nini Denis hebu tuambie?”Dolan alimtwanga swali kwa mshangao. “Denis.”Dick aliita,Denis aligeuka na kumtazama.Uso wake ulionesha waziwazi huzuni aliyokuwa nayo.Hakuzungumza chochote badala yake akawapa wenzake simu yake na kuwaonesha ule ujumbe ulitoka kwa Vivian.Walisoma huku wakiwa wanapiga hatua kuingia ndani ya hoteli. “Denis usiwaze sana sisi tutaongea na Vivian wala hakuna tatizo.Huu ni wivu tu ndiyo unaomsumbua kutokana na mapenzi aliyokuwa nayo kwako.”Dolan alimkimbilia rafiki yake aliyekuwa mbele na kuanza kumtia moyo.Denis hakujibu kitu kwasababu walishafika kwenye chumba alichokuwemo Bi Zena.Aligonga mlango mara mbili na kusubiri jibu toka ndani.Baada ya kuona kimya aliamua kugonga tena sambamba na kupaza sauti yake kumwita mama huyo. “Mama!mama!Bi Zena!Bi Zena!”Kimya. “Una hakika kwamba ni hapa?”Dick aliuliza baada ya kuanza kupata wasiwasi. “Ni hapa hapa kaka.”Denis alijibu kwa sauti ya unyonge. “Hebu jaribu kumpigia tena simu.” “Hapatikani.” “We jaribu.”Denis alipokea simu toka kwa Dolan na kuipiga namba ya Bi Zena.Jibu lilikuwa lile lile kwamba haipatikani.Denis alishusha mkono wake kinyonge kuonesha kwamba amekata tamaa.Kuona hivyo,Dick akaamua kubonyeza kitasa cha mlango huo.Kwa bahati nzuri mlango haukufungwa kwa ndani hivyo Dick alipousukuma kidogo tu ukafunguka. “Mungu wangu!nini hiki?” “Haaah!Mamaaaa!” “Bi Zena!Bi Zena!Mungu wangu!Umekumbwa na nini mama yangu?”Kila mtu alipigwa na butwaa kwa hali waliyoikuta mule chumbani. Bi Zena alikuwa amelala chini badala ya kitandani.Alikuwa ameuchapa usingizi fofofo hivyo hakuweza kujitambua.Juu ya meza iliyokuwa mule chumbani kulikuwa na chupa tano za pombe kali zilizokuwa tupu na moja ilikuwa nusu.Baada ya Denis kuondoka hiyo jana yake alipomfikisha katika hoteli hiyo,Bi Zena aliagiza wine chupa sita na kuanza kujitibu taratibu usiku kucha.Pombe hizo zilipomzidia aliishiwa nguvu na kudondoka chini ambapo aliuchapa usingizi hapo hapo mpaka akina Denis walipowasili kwa muda huo. Simu yake ilikwisha chaji ndiyo maana akawa hapatikani.Kitendo cha kunywa pombe kupita kiasi kilimfanya mama huyo kujisaidia haja kubwa na ndogo pale pale bila ridhaa yake.Denis alisikitika sana kutokana na suala hilo.Alijisikia aibu mbele ya rafiki zake ambao waliona kinyaa na kuamua kutoka nje ya chumba.Hali ya Bi Zena ilikuwa mbaya sana,moyo wake ukawa unadunda kwa mashaka.Ilibidi Denis ajitoe ufahamu na kuamua kumbadilisha mama huyo nguo,kuanzia nguo za ndani na kumvalisha nyingine zilizokuwa kwenye begi lake. Baada ya hapo alimbeba na kutoka naye nje kisha akamwingiza ndani ya gari na kumpeleka Muhimbili huku rafiki zake wakimfuata nyuma.Alipatiwa huduma na baada ya saa kadhaa alizinduka na kuanza kushangaa.Alipouliza amefikaje eneo lile Denis hakumficha hata chembe.Alimwambia kila kitu na alimweleza jinsi alivyokasirishwa na kitendo hicho kilichomtia fedhea kwa watu.Bi Zena aliomba msamaha na kuahidi kutorudia tena kufanya kitendo kama hicho. Denis alimsamehe lakini kwa sharti la kumrudisha Tanga mpaka pale binti yake atakapopona ndipo aonane naye.Bi Zena alikubali bila kipingamizi na alifurahi sana kusikia hivyo kwani aliona ndiyo atakuwa huru kutanua.Hakuwa na wasiwasi juu ya hali ya mwanaye.Aliamini Denis atamhudumia kwa kila kitu mpaka atakapopona na kumrejesha nyumbani.Hata hivyo Denis hakumwambia kwamba kuna safari ya kumpeleka Shaimaa nje kwa matibabu.Aliamua kufanya hivyo ili kuepuka kero za mama huyo kwani aliamini angeng’ang’ania kubaki na kuendelea kumtia aibu zaidi pale mjini. Siku iliyofuata Bi Zena alienda kumuaga mwanaye na kumdanganya kuwa anakwenda kuitazama familia mara moja na kurejea.Shaimaa alisikitika sana lakini hakuwa na jinsi kwani waliokuwa wamebaki nyumbani ni watoto wake pamoja na babu yao hivyo pia uangalizi wa bibi yao ni muhimu zaidi.Siku hiyo hiyo Denis alimpandisha Bi Zena basi na kumkatia tiketi kisha akampatia pesa za kutosha kwaajili ya matumizi ya familia na kuondoka zake. Baada ya hapo Denis alianza kupanga mikakati ya safari ya kumpeleka Shaimaa nchini India kwa matibabu.Wakati wakiendelea na mipango hiyo vile vile alijaribu kuzungumza na mchumba wake ili kumwelewesha kwa kile alichokifanya lakini wapi!Vivian alishikilia msimamo wake wa kuachana na Denis kutokana na ukaribu aliokuwa nao kwa Shaimaa.Jambo hilo lilimkera sana likawa linamhuzunisha kila wakati. Alitumia kila mbinu kusuluisha tatizo hilo hata hivyo aligonga mwamba.Kuna kipindi alitaka kukata kabisa msaada kwa Shaimaa ili kulinusuru penzi lake lakini moyo ulimsuta.Hali ya binti huyo ilimfanya ajawe na huruma ndiyo maana akajitoa mhanga kwaajili yake.Nyumbani kwa akina Denis walimsusa akawa anahangaika peke yake.Hakuona shida kwasababu walikataa kutambua matatizo aliyokuwa nayo binti huyo.Wao walishikilia msimamo wa yale Shaimaa aliyomfanyia Denis kwa kumsingizia kesi isiyokuwa ya kwake. Ingawaje ilimuumiza na kumsababishia matatizo lakini aliliweka pembeni na kuamua kumsaidia kwa moyo.Baada ya kila kitu kukamilika ikiwemo kuzijua gharama za usafiri pamoja na matibabu,Denis alifanikiwa kumpeleka Shaimaa nchini India kutibiwa.Kwa majaliwa ya Mwenyezi Mungu,Shaimaa alifanikiwa kuungwa miguu yake na kupona kabisa.Walirejea Tanzania wakiwa wenye furaha na amani tele.Denis aliishi na binti huyo nyumbani kwake maeneo ya Mikocheni akifanya naye mazoezi asubuhi na jioni ili kuimarisha misuli ya miguu yake. Walipokuwa wanaishi katika nyumba hiyo kila mtu alilala chumba chake akimheshimu mwezake kama kaka na dada.Lakini kadri siku zilivyozidi kusonga mbele Shaimaa aliipoteza furaha aliyokuwa nayo aakwa ni mtu wa huzuni kila kukicha.Denis alisikitishwa mno na jambo hilo.Alijaribu kumhoji taratibu il ajue anasumbuliwa na nini lakini Shaimaa alikuwa mgumu wa kuweka tatizo lake wazi. Denis alikuwa kijana mwenye moyo wa ajabu sana.Aliendelea kuwatumia wazazi wa Shaimaa fedha za matumizi kila wiki.Aliamua kufanya hivyo kwasababu tegemeo lao bado halijarudi katika hali yake ya kawaida kabisa.Alijua kuwa Shaimaa atakapoimarika zaidi atarejea nyumbani kwao kuendelea na shughuli zake za kawaida.Siku moja jioni walipokuwa mazoezini Shaimaa alimwambia Denis kuwa kuna kitu anataka kumwambia.Walitafuta sehemu ya kupumzikia na kwenda kutulia. “Uuuwi!daaa!nimechokaje!”Shaimaa alikaa chini kwenye kiwanja kilichokuwa na majani ya kijani kibichi kilichokolea sana.Alionekana amechoka mno baada ya kufanya mazoezi kwa muda mrefu. “Mmmh!uvivu huo,huna lolote.Yaani leo wala hatujajifua sana halafu unasema umechoka!”Denis alimshangaa Shaimaa. “Loo!Mwenzangu kwa leo inatosha.Au unataka niwe mwana bondia?Ha!ha!ha!ha!hapana kwa kweli,utaniua bure!Na mbio zote hizo halafu useme hakuna tulichokifanya!Hebu kaa chini kwanza tuongee.” “Ila Shaimaa acha uvivu,mazoezi ndiyo yanaimarisha misuli ya mwili.We endelea kuwa mlenda mlenda tu.”Denis alizungumza huku akiwa anaketi kwaajili ya kumsikiliza Shaimaa. “Heeh!mwenzangu!We mwanaume mi mwanamke,tusipelekane kijeshi babu wewe!” “Ha!ha!ha!ha!muone kisura chake.” “Kimefanya nini?” “Kama cha panya.” “Haaah!halafu Denis sitaki uchokozi wako.” “Kwani uongo?” “Ndiyo.” “Haya basi yaishe mama.” “Sitaki,nimenuna.” “Haa!wanaonuna wanasema au utaona vitendo tu!” “Ndiyo hivyo basi mimi nimeamua kusema.” “Ha!ha!ha!ha!ha!bichwa lile.” “Kama lako.” “Wee!ungepata kichwa kama changu si ungeringa sana.” “Kwa kichwa gani ulichokuwa nacho?Mbichwa kama Fenesi.” “Ha!ha!ha!ha!kweli we mwanamke umenichoka.” “Mmh!jamani siwezi kukuchoka Denis.” “Haya mama.Ukija tena hunikuti huku.” “Utaenda wapi?” “Nahamia zangu Mkuranga kwenye nyumba yangu nyingine.” “Kwanini?” “Nimeamua tu.” “Kwani nyumba yako ya Mikocheni siyo nzuri?” “Ni nzuri sema tu nimeamua kubadilisha mazingira.” “Haya baba mimi sikuwezi.” “Utaniwezea wapi?”Baada ya matani ya hapa na pale Shaimaa alianza kumweleza Denis kile alichomwahidi.Kwanza alikohoa kidogo kutengeneza koo lake kisha akainua uso na kumtazama Denis.Denis alifanikiwa kuiona huzuni aliyokuwa nayo binti huyo.Alijaribu kutega sikio kwa makini ili asikie vizuri dukuduku lake. ******** Itaendelea....Nashukuru kwa ufuatiliaji wako wa hadithi hii....Naamini unaendelea kujifunza mengi na pia unaburudika vya kutosha.Nakutakia siku njema na Mungu akubariki sana. ******** Kwa maoni au ushauri napatikana kwa namba 0655089197/0766123623 Author : Unknown Share this Related Posts