STORY-PENZI LA MSHUMAA
MTUNZI-MZIRAY F.M.
SEHEMU YA 17
Ilipoishia sehemu ya 16
Baada ya mawazo hayo
kuanza kupotea ndani ya kichwa cha Denis,taratibu usingizi ukaanza kumnyamelea
mdogo mdogo.Hakujua hata amelala saa ngapi lakini alikuja kushtuka baada ya
kudondokewa na matone ya maji baridi usoni.Alipofungua macho yake alimuona
Vivian akiwa na glasi ya maji mkononi.
Sasa endelea....
“Denis amka acha
uvivu.Unajua sasa hivi ni saa ngapi?”Vivian alimwambia hayo Denis baada ya
kumwangalia kwa macho yaliyokabwa na usingizi.
“Kwani saa
ngapi?”Denis aliuliza kivivu.
“Saa mbili.”
“Saa mbili!Mbona
umeshapendeza saa hizi,unakwenda wapi?”Denis alimshangaa mchumba wake aliyekuwa
anawaka ndani ya mavazi yake ya heshima.
“Ndiyo tunaondoka
hivyo.Akina Brenda wamenipigia simu na kuniambia kuwa wameshajiandaa kwa
safari.”
“Duuuh!mbona
hawajanishtua?”
“Wamekupigia simu
zaidi ya mara nne sema tu tulikuwa tumelala na simu yako sijui umeiweka
wapi?Kuona hupokei ndiyo wakaamua kunipigia mimi.”Denis alipopata taarifa hizo
alikurupuka toka kitandani na kujifunga taulo.
“Simu yangu sijui nimeiweka
wapi?Hebu piga namba yangu nisikie inapoitia.”Vivian alichukua simu yake na
kumpigia Denis. “Inaita?”Denis aliuliza
“Ndiyo.”
“Inaitia wapia sasa
mbona siisikii?”
“Nasikia mlio kwa
mbali sijui ni wapi.Hebu angalia kwenye suruali yako.”Denis alipokwenda kucheki
ndani ya suruali yake alikuta simu iliyokuwa na missed calls tano.Mbili za
Dick,moja ya Brenda,nyingine ndiyo hiyo ya Vivian aliyepiga muda huo huo
walipokuwa wanaitafuta simu hiyo.Moja ilikuwa ni namba ngeni kabisa katika simu
ya Denis.Aliachana nayo akaingia bafuni kusafisha mwili wake.
Alipotoka alivaa nguo
zake kisha akafuatana na Vivian mpaka nje ya hoteli.Alipiga namba ya Dick ikawa
inatumika akaamua kumpigia Dolan.Alimwambia kuwa Vivian yupo tayari kwa safari
hivyo wampitie pale hotelini.Baada ya dakika tano akina Brenda waliwasili pale
Dolphin hoteli.Brenda akiwa na wenzake walimkumbatia Denis na Vivian kwa furaha
ya ajabu.
“We Denis ulikuwa
umelala usingizi wa pono nini?Mbona tumekupigia simu mara kibao hujapokea?”Dick
alianza kumshambulia Denis kwa maswali.
“Ha!ha!ha!ha!ha!nisameheni
jamani nilikuwa nimesahau simu kwenye suruali yangu.”Denis alijitetea.
“Umesahau simu wapi
sema mahaba yalikubana.”
“Ha!ha!ha!ha!ha!ha!”
“Waooooh!Dolan hapo
umeongea.Maana Vivian akimkamata Denis kwenye kona yake huwa hatoki kaka yangu
huyu.”Winfrida aliunga mkono kauli ya Dolan na wote wakacheka kwa pamoja.Vivian
alimkumbatia Denis na kuuficha uso wake kwa aibu.
“Ha!ha!ha!ha!Vivian
twende,sisi ndiyo tunaondoka hiyo.Au umeshapata wazo la kubaki Tanga ghafla?”Brenda
alitaniana na wifi yake ambapo furaha iliendelea kutawala eneo lile.
“Huyu mwacheni
nampakia kwenye gari yangu mpya nawasindikiza mpaka Kange stendi
kuu.Tukishafika hapo ndiyo atakuja kupanda hicho kibatari chenu.”Denis
alimng’ang’ania mchumba wake na kuwaringishia ndugu zake.
“We jishaue tu na
Range Rover lako.Tungejua tusingekuja kukutoa,ungeozea mahabusu.”Brenda naye
aliingiza utani wake na kufufua vicheko kwa wenzake.
“Ha!ha!ha!ha!ha!ha!hilo
nalo neno.”
“Ha!ha!ha!ha!uliona
jinsi Vivian alivyochimbwa mkwara na yule afande?”Dick alitoa la kwake.
“Ha!ha!ha!ha!alikuwa
anatetemekaje!Na ukome kuropokaropoka ovyo.Kama siyo huyu mumeo kujitoa muhanga
ungekuta na wewe upo ndani.”Brenda alizidi kupigilia msumari.Baada ya utani wa
hapa na pale waliingia kwenye gari na kuanza safari ya kurudi
Dar-es-salaam.Walipofika maeneo ya Kange stendi mpya Denis alimshusha Vivian
ambapo alienda kuingia kwenye gari walilokuja nalo Tanga.
“Mhudumie vizuri
mgonjwa wako feki.”Winfrida alichungulia dirishani na kumrushia dongo kaka
yake.
“Nendeni zenu
huko.Kwaherini jamani nawatakia safari njema.Bye!bye!msijali wiki ijayo
nitakuja huko.”Denis aliagana na ndugu zake haoo wakayoyoma zao.Baada ya hapo
Denis aligeuza gari na kuanza kurejea hotelini mdogo mdogo.Wakati akiwa kwyene
gari Denis alitoa simu yake akawa anapitiapitia mambo fulani yanayohusu
biashara zake.Mara akakumbuka kuwa kulikuwa na namba mpya iliyompigia asubuhi
lakini hakuipokea.Aliitafuta hiyo namba kwenye orodha ya simu zilizoingia na
kuikuta.Alibonyeza kitufe cha kupigia na kuiweka sikioni.Iliita kidogo tu mara
ikapokelewa.
“Hello!habari yako
kijana?”Upande wa pili ulimjulia hali Denis baada ya kupokea simu.
“Habari ni nzuri
tu,shikamoo.”Denis alisalimia na kutulia.
“Marahaba.Sasa ni
hivi,mimi ni Mzee Kambi baba yake Shaimaa.”Upande wa pili ulijitambulisha.
“Baba yake
Shaimaa,mmh!Shaimaa!Bado sijakupata vizuri,Shaimaa wa wapi?”Denis alitaka
ufafanuzi zaidi.
“Nipo Bombo
hospitali.Ni baba wa huyu binti uliyempa ulemavu.”Mzee alizungumza kwa ukali
kidogo baada ya kuona kuwa Denis hamwelewi.
“Ooooh!nimeshakupata
vizuri.Samahani sana mzee wangu,hilo jina la Shaimaa kidogo bado sijalishika
ndiyo maana ikawa shida kukufahamu kwa haraka.Ehe!vipi hali ya mgonjwa?”
Japokuwa Denis aliumia
baada ya Mzee Kambi kuendelea kumshutumu kuwa yeye ndiye aliyemgonga binti
yake,lakini alijikaza kiume na kuzungumza naye kistaarabu.
“Kwa kweli hali siyo
nzuri hata kidogo.Tunakuomba hapa hospitali mara moja.”
“Kwani kuna tatizo
gani mzee?”
“Tatizo lipo tena
kubwa sana kuhusu binti yangu.”
“Haaa!kuna usalama
kweli hapo?”
“We njoo kila kitu
utakuja kukijulia huku huku.”
“Haya nakuja sasa
hivi.”Denis alishtuka sana baada ya kuambiwa kuwa hali siyo nzuri kule
hospitali.Alikanyaga mafuta na kuongeza mwendo kuelekea mjini.Kabla hajaikamata
barabara ya Raskazoni,Denis alipaki gari pembeni na kuanza kutafakari. “Hivi
kuna usalama kweli huko ninapokwenda?Isijekuwa najitumbukiza mwenyewe kwenye
mdomo wa Simba!Sijui niende,sijui nisiende?Daah!hii mbona kazi.Nilishajihukumu
mimi mwenyewe acha tu niende.”
Denis aliingiza gari
barabarani na kuongeza mwendo kuelekea Bombo hospitali.Japokuwa hakuwa na
uhakika wa huko aendako lakini ilimlazimu kwenda hivyo hivyo kichwa kichwa
tu.Alipofika hospitali alipokelewa na huzuni iliyokuwa imewatawala wazazi wa Shaimaa.
“Shikamooni wazee
wangu.”Denis alisalimia kwa heshima.
“Unamsalimia nani?Kama
hizo shikamoo zingekuwa mali ungekuta sasa hivi tunamiliki ghorofa.”Mzee Kambi
alimkaripia Denis kwa hasira.
“Aaaah!jamani,mimi si
ninawasalimia tu!Kwani kuna tatizo gani?”Denis alipigwa na butwaa.
“Hebu tupishe huko
mnafki mkubwa wewe.Wewe si ndiyo umemsababishia mwanetu hayo matatizo.Na kama
akifa lazima umle nyama labda mimi siyo Bi Zena.”Mama yake Shaimaa naye
alilipuka kama petrol.
“Bado sijakuelewa
mama,unamaanisha nini kusema hivyo?”
“Bado hujanielewa
eeeh!Utatuelewa tu baada ya tegemeo letu kufa.”Denis alibaki njia panda asijue
wale wazee wanamaana gani kusema vile.Moyoni aliumia sana kwa kuendelea
kushutumiwa kwa kosa lisilomhusu.Nani anaweza kusimama na kumtetea?Ukweli wote
alikuwa nao Shaimaa ambaye ndiyo anaweza kubadilisha mawazo ya watu juu
yake.Lakini ndiyo hivyo,msichana huyo bado aliendelea kushikilia msimamo wake
kuwa Denis ndiye kahusika na ajali yake.Aliwatazama wale wazee walivyokuwa
wanamshumbulia kwa maneno ya lawama hadi akajikuta amedondosha chozi la
uchungu.
“Unajifanya
kulia!Unalia kitu gani?Unajiliza unafki tu hapa.Kisa umeona una fedha basi
ukaamua kuiharibu nguzo yetu ya familia.Kwahiyo sasa hivi roho yako
nyeupee,furaha imekutawala.Azma yako ya kutumia pesa zako vibaya kwa
kuwanyanyasa wasiokuwa nacho imeshatimia sasa.Usijifnye kumlilia mwanangu
wakati wewe ndiyo umemwingiza katika matatizo haya kwa makusudi.”Mzee Kambi
aliendelea kumzonga Denis huku akiwa kaukunja uso wake kwa hasira.Hata hivyo Denis
hakujibu chochote,aliamua kuingia chumba cha daktari ili akaulizie hali ya
Shaimaa.
“Haa!kijana umerudi
tena?karibu sana.”Denis alipoingia kwa daktari alikumbana na yule dokta
aliyemuitia polisi wakaja kumkamata.Alitamani arudi lakini alipoikumbuka hali
aliyoiacha nje ikamlazimu kuzungumza tu na yule daktari.
“Habari siyo nzuri
dokta,nataka nifahamu maendeleo ya Shaimaa.”Denis aliuliza akiwa wa motomoto.
“Kwanza umekutana na
wazazi wa huyo binti?”Dokta aliuliza.
“Ndiyo.”
“Umeona hali zao?”
“Dokta niambie huyo
binti anaendeleaje.Habari za wazee wake za nini sasa hapa?”Denis alikasirishwa
na maswali ya yule daktari.
“Hali ya wale wazee
ndiyo kioo cha hali aliyokuwa nayo binti yao.”
“Dokta
sijakuelewa,hebu nenda moja kwa moja kwenye pointi.”Denis alizidi kupaniki
kutokana na maelezo ya yule daktari.
“Shaimaa yupo katika
hali mbaya sana na kama jitihada zisipofanyika mapema anaweza akapoteza uhai
wake.”Dokta alimpasulia Denis jipu alilolitaka.
“Unasema kweli dokta?”
“Ndiyo.”
“Kwahiyo unashauri
nini kifanyike?”
“Anatakiwa ahamishiwe
Muhimbili haraka iwezekanavyo ili kunusuru maisha yake.”Kutokana na mvunjiko
alioupata Shaimaa,madaktari wa pale Bombo hospitali,walishindwa kuiunganisha
miguu yake vizuri hivyo wakatoa ushauri wa kumhamishia mgonjwa huyo katika hospitali
ya taifa Muhimbili iliyopo jijini Dar-es-salaam.
“Daah!ama kweli huu
mtihani.”Denis alishusha mabega yake chini kwa unyonge.
“Tena mtihani mzito
kweli kweli kwa wazazi wa huyu binti siyo kwako.Umewatia dosari ya
maisha.Wameniambia kuwa huyo binti ndiyo tegemeo lao pale nyumbani.Wao hawana
shughuli yoyote ya kuwaingizia kipato.Wamesema kuwa Shaimaa ndiyo alikuwa
anatoka na kwenda kubangaizabangaiza mitaani na kuwaletea chochote kitu.Tangu
mtoto wao apate ajali hawajaingiza chochote mdomoni na ukizingatia wanaishi na
mabinti wadogo wawili wanaosoma.Wamekilaumu sana kitendo ulichomfanyia binti
yao ambacho kimeathiri familia nzima.Kwahiyo kijana tambua kuwa laana ya wazee
hao itakusumbua maisha yako yote.”
************
Je nini kitaendelea?Usikose kufuatilia mwendelezo wa hadithi hii iliyojaa visa na mikasa ya kusisimua.Nakutakia siku njema na Mungu akubariki sana.
********
Kwa maoni au ushauri napatikana kwa namba 0655089197/0766123623