STORY-PENZI LA MSHUMAA
MTUNZI-MZIRAY F.M.
SEHEMU YA 7
Ilipoishia sehemu ya 6
Baada ya Mzee Mwamba
kuzungumza hayo kila mtu alitega sikio lake kusikiliza kauli ya Denis.Denis
alinuua macho yake na kumtazama kila mmoja usoni halafu akatiisa kichwa kwa
masikitiko. “Vivian.”Denis aliita kwa upole.
“Abee.”Vivian
aliitikia huku akiwa na wasiwasi mkubwa moyoni.
“Nimeshakusamehe hivyo
unaweza kurudi kwenu.”Baada ya Denis kutamka maneno hayo aliyatupa macho yake
pembeni.
“Haah!sasa arudi kwao
kivipi?”Winfrida alishindwa kumwelewa kaka yake.
Sasa endelea..........
“Kwani alivyokuja hapa
si alisema amekuja kuomba msamaha!Ameshasamehewa sasa anasubiria nini
hapa?”Denis alizidi kuwashangaza watu kutokana na maneno yake ya kejeli.
“Kwahiyo huyo ndiyo
wifi yetu,siyo Shaimaa tena?”
“Mama unamuona Brenda
anavyonitafuta?Brenda chunga mdomo wako nitakuja kukuharibu.”Kauli ya Brenda
ilizidi kumtibua Denis aliyewaka kama moto wa mabua.
“Denis mwanangu,mbona
hatukuelewi?Unasema kuwa umeshamsamehe Vivian halafu unamwambia
aondoke!Inamaana unamfukuza mkwe wangu au?”Mama mtu aliamua kuvunja ukimya
aliokuwa nao.
“Mkwe wako
kivipi?”Denis alimtupia mama yake swali.
“Sasa kama
umeshamsamehe Vivian maana yake si mkeo mtarajiwa!Ndiyo maana mimi namwita mkwe
wangu.”
“Hivi mama mimi
niwaeleze mara ngapi?Nimeshawaambia kuwa sitoweza kumuoa Vivian,mbona hamtaki
kunielewa jamani!”Denis aliongea kwa jazba mbele ya wazazi wake.
“Hivi Denis umelogwa
au?Tumeshakuambia huyu binti ndiyo mwenye sifa sahihi za kuwa mkeo.Unaenda
kuhangaika na wasichana wa Tanga wa kazi gani?Sikiliza nikuambie,huyu ndiye
mkwe wetu tunayemtambua huyo mwingine hatumjui.”Mzee Mwamba alizungumza kwa
ukali baada ya kuona kuwa Denis hataki kuelewa.Hata hivyo Denis aliendelea
kushikilia msimamo wake kama kawaida.Hakuvipa nafasi vitisho vya wazazi wake
viweze kubadilisha maamuzi yake.
“Jamani!nyie ni wazazi
wangu na ninapaswa kuwahishimu sana,ila kwa hili,mtanisamehe bure.Kama
mnamtambua Vivian kuwa ndiyo mkwe wenu,endeleeni kumtambua hivyo hivyo lakini
kwa upande wangu Shaimaa ndiyo kila kitu katika maisha yangu.Na kwa taarifa
yenu nilichokifuata hapa ni kuwajulia hali sambamba na kuwaeleza kuwa natarajia
kufunga ndoa na mchumba wangu wiki ijayo.Haijalishi kama mtanipa baraka zenu au
hamtanipa.Haijalishi kama mtahudhuria kwenye harusi yangu ama la!lakini ndoa
lazima ifungwe.”
Denis aliamua kutumbua
jipu hadharani.Hakutaka kufanya kificho chochote,alieleza kitu alichopanga
katika maisha yake ya ndoa.Baada ya kusikia hivyo,Vivian aliinama chini na
kuanza kudondosha machozi ya uchungu.Alijutia alichokifanya ndani ya nafsi yake
kwa kukurupuka bila kufanya uchunguzi wowote na matokeo yake ndiyo hayo ya
kunyang’anywa tonge mdomoni.
“Haah!kaka,unafunga
ndoa wiki ijayo bila hata kufanya maandalizi yoyote?”Winfrida alishtushwa na
taarifa ya Denis.
“Hilo ni jibu unapigia
mstari,siyo swali.Unataka nifanye maandalizi gani wakati nyie wote hapa
mmenipinga?Sihitaji kamati wala sina haja na ndugu yeyote.Mkitaka mtakuja
msipotaka basi.Kifupi ni kwamba,Shaimaa ndiyo ubavu wangu wa pili.Vivian
akatafute mwanaume mwingine anayeona ni mwaminifu kuliko mimi.”Denis aliwaacha
vinywa wazi wajumbe wote waliokuwepo kwenye kikao kile kisichokuwa rasmi.
“Lakini kaka…….”
“Lakini nini?Tena
ninyi ndiyo msiniingilie kabisa maana mawifi mnasifika dunia nzima kwa kuharibu
ndoa za kaka zenu.Kama mmeshindwa kuniunga mkono,sihitaji mazoea yoyote na
nyie.Kuna hata siku moja mimi nilishawahi kuwafuata na kuwachagulia
mwanaume?Shikeni hamsini zenu na mimi nishike zangu.”
Denis alizungumza kwa
hasira mpaka mate yakamkauka mdomoni.Uso wake aliukunja kama Nyati akitamani
kuwameza dada zake walioonesha kumpinga waziwazi.Kuona hiyo,Vivian aliinuka kwa
hasira huku machozi yakifunika macho yake na kuamua kutoka nje ya nyumba ile.
“Vivian!Vivian!Wifi
njoo unakwenda wapi?”
“Vivian mwanangu
usiondoke.”
“Wifi njoo we ndiyo
mwanamke wa nguvu hapa.”Bi Asma na wanaye wa kike walijaribu kumsihi Vivian
aisondoke lakini tayari binti huyo alishafika nje.Brenda aliamua kumfuata na
kumbembeleza lakini wapi!Hasira zilimkaba kooni akawa anazungumza kwa jazba.
“Sitaki!sitaki!Niache
Brenda.Kaka yako ameshaamua kuoa hivyo mimi sina tena thamani katia familia
yenu.Amekataa kunisamehe kwa kosa nililomfanyia ilihali nimeshamuomba
radhi.Namtakia maisha mema katika ndoa yake,Mungu ambariki sana.”Baada ya
Vivian kuzungumza maneno hayo kwa uchungu,alitoka mbio na kuyoyoma zake na
kumwacha Brenda akiendelea kumwita bila mafanikio.
“Vivian!Vivian
usiondoke jamani!Tutazungumza vizuri na Denis ataelewa tu.”Brenda aliishia
kuzitazama nyao za Vivian ilihali mwili wa binti huyo haukuwepo eneo lile.
“Unaona sasa kaka Denis ulichokifanya!Mtoto wa watu anakupenda yule sijui
kwanini unamfanyia vitu vya ajabu namna hiyo?”Brenda aliporudi ndani moja kwa
moja akaanza kumporomoshea lawama kaka yake.
“Naona nini?Mwache
aende zake.Eti ananipenda!Angekuwa ananipenda angenisingizia huo ujinga
wake?Anafikiri mimi ni malaya kama yeye.”
“Denis,maneno gani
hayo ya kishenzi unazungumza mbele yetu?”Mzee Mwamba alikasirishwa sana na
kitendo cha Denis kuropoka maneno yake yasiyofaa mbele ya wazazi wake.
“Lakini Denis ujue
wivu ndiyo uliomfanya Vivian akuwazie vibaya juu ya uhusiano wako na
Shaimaa.Siku zote mwenye mapenzi ya dhati kwako lazima awe na wivu juu
yako.Hakukusudia kusema kwamba Shaimaa ni mpenzi wako.Ule ukaribu uliokuwa naye
ndiyo uliomponza Vivian.”Brenda alijaribu kumtetea Vivian kwa Denis lakini
wapi!
“Sikiliza
nikuambie,tambua kuwa anayemuwazia mwenzie mabaya basi naye hufanya hivyo
hivyo.”
“Si kweli.”Brenda
alibisha.
“Hata kama usipokubali
lakini ukweli ndiyo huo.Kwa kuwa alinisingizia mpaka akasema tuachane,nami
nimeamua kufanya kweli na wiki ijayo nafunga ndoa na Shaimaa.”Denis aliendelea
kushikilia msimamo wake.
“Hivi Dickson mwanangu
unashindwa kuzungumza na ndugu yako na kumshauri kuwa huko anapokwenda
anapotea.”Mama yake Denis aliamua kuvunja ukimya aliokuwa nao.Alimgeukia Dick
aliyekuwa kimya muda wote na kumchangamsha kwa swali hilo.
“Nimeshazungumza sana
na Denis lakini moyo wake umekuwa mgumu kubadilika.Ujue mapenzi yana nguvu sana
na mtu akishapenda huwa hashauriki tena.Marafiki zake wengi tumemsihi mara
nyingi tuwenzavyo lakini tumefua dafu.Sasa hivi tumekaa kimya na kuyapisha
maamuzi yake yafanye kazi.”Dick aliongea maneno machache sana ili asionekane
kama ni mpinzani kwa rafiki yake ilihali ameshakubali kuwa sambamba naye katika
ndoa yake.
“Lakini huoni kama
anapotea?”Mzee Mwamba naye aliamua kumuuliza Dick swali la mtego.
“Ha!ha!ha!ha!Ujue huyu
ni mtu mzima na upeo mkubwa mno wa kufikiri.Ni msomi,anajua lipi zuri na lipi
baya.Hivyo mimi sioni kama anapotea kwasababu yeye ndiyo mwamuzi wa mwisho na
kila mtu huwa anajichagulia maisha yake mwenyewe.”
“Ha!ha!ha!ha!sisi
tunaona unaegemea upande wake kwasababu ni rafiki yako.Hata kama mtu ana uhuru
wa kujichagulia maisha yake mwenyewe lakini ushauri nao ni mzuri hasa ushauri
wa wazazi katika kufanikisha malengo yake.”Safari hii Mzee Mwamba alizungumza
kwa upole wa hali ya juu kitu kilimshangaza kila mtu mule ndani.
“Ni kweli kabisa kuwa
wazazi ni muhimu sana katika maisha ya kijana wao hasa busara na hekima zao
zinahitajika kwa kiasi kikubwa mno ili kufanikisha malengo bora ya mtoto.Hata
hivyo,si kila ushauri wa wazazi huwa sahihi.Wakati mwingine inabidi kuwapa
watoto nafasi ya kufanya maamuzi yao wenyewe.Kwa mfano katika suala hili la
ndoa,Denis ndiyo ataenda kuishi na huyo mwanamke wake.Wala sisi hatutahusika
kwa namna moja ama nyingine.
Japokuwa inasemekana
kuwa wazazi wana maono ya kuona kitakachotokea mbele lakini mkimlazimisha Denis
amuoe mwanamke ambaye hajamridhia,basi ndoa yake itakuwa ya mvurugano zaidi ya
hii anayoitaka yeye.Hatoishi kwa raha kwa kuwa mwanamke aliyemuoa si chaguo
lake bali ni la kwenu.Sasa hamuoni kama mtakuwa hamjamtendea haki hapo?”Kila
mtu alizishangaa busara za Dickson.Hakuna mtu aliyeamini kama kijana huyo
angeweza kuzungumza maneno yaliyoshiba hekima namna hiyo.Mara nyingi tumezoea
kwamba wazee ndiyo wanaweza kutoa ushauri kama huo kuhusiana na masuala ya
ndoa.
“Dickson.”
“Naam mzee.”
“Wewe umeoa?”Mzee
Mwamba aliuliza kwa mshangao
“Hapana mzee
wangu.”Dick alijibu kwa heshima.
“Yaani jinsi
ulivyozunguza kwa ustadi wa hali ya juu utadhani upo kwenye ndoa zaidi ya miaka
kumi.Hebu tuambie umeyapata wapi yote hayo?”
“Ha!ha!ha!ha!ha!”
“Ha!ha!ha!ha!ha!baba
bwana.”
“Haaah!baba Denis
mbona unamuuliza kijana wa watu maswali mengi hivyo?Au umekuwa polisi siku hizi?”Kila
mmoja aliangua kicheko baada ya Mzee Mwamba kutaka kujua Dick alizipata wapi
busara alizokuwa nazo.Bi Asma ndiyo aliamua kumtwanga mumewe swali kutokana na
kuzidi kumwandama Dickson.
“Jamani!mimi nataka
nijue tu!Kwani kuna ubaya kijana?”Furaha ilianza kuinyemelea ile nyumba
taratibu baada ya vurumai la robo saa iliyopita kutulia.
“Ha!ha!ha!ha!hakuna
ubaya wowote ule mzee wangu.Kwanza sitaki kuamini kuwa kama nina busara nyingi
kiasi hicho.Ninyi wazee wetu ndiyo mna busara za kutosha kwasababu mmezaliwa
muda mrefu na mmekumbana na changamoto za aina mbalimbali kushinda sisi.Hata
hivyo suala la kuwa na desturi za kusoma vitabu mbalimbali linatujengea uwezo
wa kujifunza mambo mengi.Ndiyo maana Mapadri wana uwezo wa kutoa ushauri ama
kuwafungisha watu ndoa ilihali wao hawaoi.Yote hiyo ni kwasababu ya maarifa
waliyoyapata toka vitabuni.”Elimu ya chuo kikuu aliyokuwa nayo Dick ndiyo
iliyomwezesha kupambanua mambo vizuri namna hiyo.
“Ehee!umenikumbusha
kitu.Sasa mwanangu umeamua kumuoa huyo binti wako wa Kitanga na kumkataa
Vivian.Hiyo ndoa yenu inafungwa katika dini gani maana nakumbuka ulituambia
kuwa Shaimaa hataki kubadilisha dini.”Mzee Mwamba aliuliza kwa shauku.
“Tumeamua kufunga ndoa
mahakamani ili kila mtu abaki katika imani yake.”Denis alijieleza kwa kujiamini.
“Mahakamani!Hivi ndoa
za mahakamani ni ndoa kweli?Sisi tumeshakuambia huyo binti hakupendi.Angekuwa
na mapenzi ya dhati kwako lazima angekubali kufuata dini yako.Mwanangu,hapo
umeruka majivu na kukanyaga moto.”Bi Asma alihamaki baada ya mwanaye kusema
kuwa anakwenda kufunga ndoa mahakamani.
“Denis,hivi una
kichaa?Sasa ndoa ya mahakamani ndiyo ndoa gani hiyo?”Winfrida naye aliamua
kutia maneno yake.
“Sikilizeni
niwaambie,suala la dini haliwezi kupima upendo alionao mtu kwa mchumba
wake.Mnaweza mkaoana watu wa dini moja na msielewane.Au kama mnaona hiyo ni
mbaya mimi nipo tayari kubadilisha dini ili tuwe kitu kimoja.”
*********
Je nini kitaendelea?Tukutane Jumatano ijayo tuweze kuendeleza hadithi hii iliyojaa visa na mikasa ya kusisimua...Nakutakia siku njema na Mungu akubariki sana.
***********
Kwa maoni au ushauri napatikana kwa namba 06555089197/0766123623
2 comments
commentsnzuriiiiiii
Replynzuriiiiiii
Reply