STORY-PENZI LA MSHUMAA
MTUNZI-MZIRAY F.M.
SEHEMU YA 10
Siku hiyo Denis
alikuwa uwanja wa ndege wa Mwalimu Julius Kambarege Nyerere akisubiria ndege
ielekeayo Tanga.Safari yake haikuwa ya Tanga tu bali alitaka pia kwenda Kenya
katika bandari ya Mombasa kushughuli gari lake lililokwama katika bandari
hiyo.Baada ya tangazo kutolewa juu ya abiria wa Tanga,Denis alimgeukia mchumba
wake na kumkumbatia huku akimpiga mabusu moto moto ya kumuaga.
“Usijali Vivian wiki
ijayo nitakuwa hapa.Nitakwenda kwanza Mombasa mara moja kuitoa ile gari yangu
na baada ya hapo nitarejea Tanga katika shughuli zangu nyingine zilizonipeleka
huko.Nikimaliza nadhani sitakuwa na sababu yoyote ya kuendelea kukaa huko bila
kazi ya msingi.”Denis alizungumza kwa hisia za mapenzi.
“Mmmmh!nitakumisi sana
mpenzi wangu.Wiki moja ni ndefu sana kwangu.”Vivian alieleza hayo huku
akimpigapiga Denis mgongoni.
“Ha!ha!ha!ha!ha!jamani
wiki moja ndefu!Mmmmh!Vivian umezidi.”
“Siyo hivyo Denis,ujue
nimezoea kuonana na wewe kila siku.Ikipita siku moja tu sijakuona nahisi
homa.Sembuse hiyo wiki moja si nitakufa kabisa.”
“Ha!ha!ha!ha!ha!usijali
Vivian muda si mrefu tutafunga ndoa na utakuwa na mimi mpaka utanichoka.”Denis
aliendelea kumpa moyo mchumba wake waliopanga kufunga ndoa miezi michache
itakayofuata.
“Ha!ha!ha!ha!nikuchoke
kwa kipi?Wala siwezi kukuchoka mpenzi wangu hata siku moja.Tena kipindi hicho
ndiyo nitakuwa mke halali wa bwana Denis,watanikomaje!”Vivian alizungumza kwa
kujiamini katikati ya kumbatio la Denis.Baada ya kuagana Denis alivuta begi
lake dogo la matairi na kuelekea katika ndege na hiyo ni baada ya
kukaguliwa.Alipofika kwenye mlango wa ndege aligeuka na kumuona Vivian akiwa
bado kasimama anamwangalia.
Alinyoosha mkono wake
na kumpungia ambapo Vivian naye alimjibu kwa kumpungia pia.Baada ya hapo Dens
aliingia ndani ya ndege na baada ya nusu saa ndege iliacha ardhi ya Dar-es-salaam
na kupaa angani.Alifika Tanga majira ya saa 6 mchana ambapo alikodi tax na
kuamuru apelekwe katika hoteli ya Dolphin iliyopo maeneo ya Kwaminchi karibu na
barabara ielekeayo kwa mkuu wa mkoa.
Mara kwa mara Denis
alipokwenda Tanga alipenda kufikia katika hoteli hiyo ama hoteli nyingine
iliyopo jirani yake inayoitwa Nyinda hoteli.Hoteli hizo zilisifika katika kutoa
huduma bora za malazi na vyakula ndani ya Jiji hilo la Tanga.Baada ya Denis
kupata chakula aliamua kuoga na kupumzika.Alichukua simu yake na kumpigia
Vivian kumjulisha kuwa amefika salama na kwa muda huo yupo hetelini anakula
kiyoyozi.Waliongea kwa kirefu sana mtu na mchumba wake wakati dakika chache tu
zilizopita walikuwa pamoja Jijini Dar-es-salaam.
Baada ya simu kukatika
Denis aliuchapa usingizi hadi jioni.Alipoamka aliamua kuusawiri mji wa Tanga
kwa kuzungukazunguka maeneo tofauti tofauti ndani ya Tanga mjini.Giza
lilipoanza kumeza jiji hilo,Denis alirejea hotelini na kutulia.Alipanga kwenda
Mombasa siku inayofuata kulitoa gari lake katika bandari ya mji huo.
Kesho yake asubuhi
Denis aliondoka kuelekea Mombasa akiwa ndani ya basi la kampuni ya
Tahmed.Walipofika Horohoro mpakani waliingia kwenye jengo la uhamiaji na
kufuata taratibu zote ikwemo kukaguliwa hati za kusafiria kisha wakaruhusiwa
kuendelea na safari.Walipofika Mombasa Denis hakutaka kupoteza muda.Alikwenda
moja kwa moja hadi bandarini na kumalizana nao ambapo alifanikiwa kulitoa gari
lake aina ya Range Rover majira ya saa 12 jioni.
Kwa kuwa muda ulikuwa
umekwenda sana basi Denis akaamua kuchukua hoteli moja ya kifahari na kulala
ili kesho yake aanze safari ya kurejea Tanga.Ilipofika asubuhi Denis aliingia
ndani ya gari lake na kuanza kukanyaga mafuta kuelekea Tanga.Alipofika Horohoro
mpakanni kama kawaida alikaguliwa na alitakiwa kuingia TRA kwaajili ya malipo
ya gari lake.Baada ya kila kitu kukamilika aliendelea na safari kwa mwendo wa
kasi.Moyo wake ulifurahi sana kufanikisha kilichompeleka huko kwani gari
alilokuwa analihusudu sasa lipo mikononi mwake.
Alipofika Tanga kabla
hajaingia hoteli aliyofiia,Denis alielekea sheli iliyopo maeneo yale ya
Kwaminchi na kujaza mafuta.Baada ya kutoka hapo alianza kurejea taratibu ili
akapumzike.Wakati akiwa anaendesha gari mdogo mdogo mbele yake kulikuwa na
pikipiki iliyokuwa inaendeshwa kwa kasi ya ajabu huku kukiwa na binti
aliyepakizwa nyuma.Kabla hawajafika maeneo ya reli ghafla yule binti aliponyoka
toka katika pikipiki ile baada ya kugonga jiwe lililokuwa linazagaazagaa
barabarani na hatimaye akadondoka chini.
Denis alishuhudia
pikipiki nyingine ikimvaa yule binti na kumtupa pembeni.Wale madereva wa
pikipiki zote mbili waliyumba barabara nzima na kusababisha ajali ya magari
mengine yaliyokuwa yanawakwepa.
Kwa bahati nzuri
walifanikiwa kuzimudu pikipiki zao na kukaa sawa ambapo ili kuepuka lawama juu
ya kile kilichotokea walivuta mafuta na kutokomea eneo lile kwa mwendo
mkali.Watu walikusanyana kumshuhudia yule binti aliyekuwa ameumia vibaya
mno.Raia wawili waliamua kupiga mkono gari ya Denis na kumwomba amwahishe yule
binti hostipali akapate matibabu ya haraka.Kutokana na uchungu alioupata Denis
baada ya kushuhudia ajali ile,aliamua kupaki gari pembeni na kutoa msaada wake.
Binti alipakiwa kwenye
gari kisha Denis akapiga moto kumwahisha katika hospitali ya Bombo iliyopo
karibu na maeneo ya Raskazoni.Alipofika katika hospitali hiyo walikataa
kumpokea mgonjwa kwasababu hakuwa na kithibitisho chochote toka polisi
kinachoonesha kuwa msichana huyo alipata ajali.
“Sasa jamani si mtoe
hata huduma ya kwanza!Inamaana hamuoni jinsi mtu alivyoumia anavuja damu miguu
yote?Masuala ya polisi si yatafuata baadae.”Denis aliwafokea wale madaktari wa
hospitali ile baada ya kugoma katakata kumpokea mgonjwa kabla hajapitia polisi.
“Kijana hapa tunafuata
utaratibu uliopangwa.Hatuwezi kumpokea huyo binti mpaka uwe na kibali toka
polisi.”Daktari mmoja alimpa Denis maelezo hayo huku akiendelea na shughuli
zake.
“Mnasema mnafuata
utaratibu wakati mtu anakufa hapa!Kwahiyo ni afadhali mtu afe kuliko kuvunja
huo utaratibu?”Denis aliuliza kwa hasira.
“Kijana haina haja ya
kupaniki.Kituo cha polisi wala hakipo mbali sana ni hapo tu Raskazoni.Ni bora
uende hapo mara moja ili mgonjwa wako aje kupata matibabu haraka.”Denis hakuwa
na jinsi,aligeuza gari na kuelekea kituo cha polisi cha Raskazoni.Baada ya kutoa
maelezo yake walimwandikia kibali cha kutibiwa na kurudi tena hospitali.
“Si unaona sasa
ulivyorahisisha kazi.Ungeendelea kulumbana na sisi mgonjwa wako si
angekufa?Kama tungemtibu hivyo hivyo halafu akatufia tungeijibu nini
serikali?”Daktari mwingine alizidi kumtia hasira Denis aliyekuwa anavuja jasho
mwili mzima kama mtu aliyemwagiwa maji.
“Mchukueni mgonjwa
acheni porojo.Nyie vipi?mbona mnakuwa kama siyo wasomi vile!”Denis alipaniki
akaanza kuwafokea kwa hasira huku mgonjwa akiwa bado mikononi mwake.Kitanda cha
magurudumu kililetwa na yule msichana akapakizwa juu ya kitanda hicho na
kusukumwa na wauguzi kuelekea hodini.Denis alipojitazama,nguo zake zilikuwa
zimechafuka damu kila mahali kutokana na kumbeba yule binti aliyekuwa anavuja
damu miguuni.
Alifanya zoezi hilo
alipokwenda polisi na pia aliporejea pale hospitalini kwasababu alikuwa peke
yake.Wale wananchi waliomsimamisha na kumuomba msaada,baada ya kumpakiza yule
binti kwenye gari hakuna hata mmoja aliyejumuika naye kuelekea
hospitali.Kutokana na hilo,Denis alifanya kila kitu mwenyewe ikiwemo
kumfungulia huyo binti faili la matibabu.
“We kaka mgonjwa wako
anaitwa nani?”Denis aliulizwa swali na nesi mmoja aliyekuwa pale mapokezi.
“Mimi sifahamu anaitwa
nani kwasababu nimeombwa tu na wananchi nimlete hapa baada ya kupata ajali
hivyo sifahamu chochote kuhusu yeye.”Denis alipoeleza kuwa hamjui huyo msichana na wala hafahamu anapoishi,ilizua
utata kidogo.
“Unasema
humfahamu!humfahamu kivipi?We si ndiyo umemleta hapa?”Yule nesi alishindwa
kumwelewa kabisa Denis.
“Sasa hapo dada yangu
usichokielewa kitu gani?Nimeshakwambia huyo binti mimi simfahamu.Nimeombwa tu
msaada wa kumleta hapa baada ya kupata ajali ya pikipiki pale maeneo ya
Kwaminchi kabla hujafika mjini.”Denis alijitetea.
“Kwahiyo hapa kwenye faili
lake tuandike nini?”Yule nesi alizidi kumwandama Denis.
*******
Je nini kitaendelea?Usikose sehemu ijayo ya mwendelezo wa stori hii..Nakutakia siku njema
*******
Kwa maoni au ushauri napatikana kwa namba 0655089197/0766123623