STORY-PENZI LA MSHUMAA
MTUNZI-MZIRAY F.M.
SEHEMU YA 16
Ilipoishia sehemu ya 15
“Basi Denis usilie
mpenzi wangu.Haya mambo tutayamaliza tukishatoka hapa.Tutazungumza kwa kirefu
na wazazi wa huyu binti tujue tunamalizana vipi nao ili turudi
Dar-es-salaam.”Vivian alimfuta Denis machozi na kumwambia akaze moyo yeye ni
mtoto wa kiume.Alimshika mkono na kusogea naye karibu na kitanda cha Shaimaa.
Sasa endelea.....
“Habari yako
binti?”Denis alimjulia hali Shaimaa.
“Kwa kweli hali yangu
siyo nzuri hata kidogo.Madokta wamesema naweza nikakatwa miguu.Uuwiii!jamani
eeh!Mimi nimeshakuwa mlemavu wa kudumu milele na milele.Nitaishije mimi na
ujana huu?”Shaimaa alizungumza huku akiwa anamwaga machozi mfululizo.Kila mtu
aliguswa na maneno yake ya uchungu.Hadi Denis aliyekuwa na hasira naye kutokana
na kumsingizia kesi isiyomhusu,huruma ilimwingia.Wakati wakiwa katika hali ya
huzuni mara nesi akaingia na kuwaambia kuwa muda wa kumwona mgonjwa umekwisha
hivyo waondoke warudi tena kesho yake..
Walipotoka nje Denis
alibadilishana namba za simu na wazazi wa Shaimaa kisha wakaondoka zao.Baada ya
hapo Denis naye akaingia kwenye gari na kuwaomba ndugu zake wampeleke hoteli
aliyofikia ambayo ni Dolphin hoteli akapumzike.Hapakuwa na umbali wowote toka
Bombo hospitali hadi maeneo ya Kwaminchi ilipo hoteli hiyo.Baada ya kuingia
hotelini Denis alienda bafuni na kujimwagia maji kisha akaenda kupata chakula
akiwa sambamba na ndugu zake.Wakati wakiwa wanaendelea kupata chakula cha
usiku,Denis aliwasimulia jamaa zake jinsi ajali ya Shaimaa iliyotokea mpaka
raia wakamsimamisha na kumwomba amwahishe binti huyo hospitali.
“Haaa!kwahiyo yeye
aligongwa na pikipiki?”Brenda aliuliza kwa mshangao.
“Ndiyo ilivyokuwa na
madereva wa pikipiki zote walifanikiwa kutoroka eneo lile.Nashangaa nilipofika
hospitali yule msichana akanigeuzia kibao na kusema kuwa eti mimi ndiyo
nimemgonga.Sijui ni kwanini ameamua kufanya hivyo?”Denis alizungumza huku akiwa
anakata msosi haraka haraka kwani tangu jana yake alipokumbana na mkasa huo
hakuingiza kitu chochote tumboni.
“Ana haja eti!tena
siyo haja ndogo,ni haja kubwa ya wiki nzima.Kama kwao hawana choo atafute pori
akajisaidie.Nyoo!anataka kuponea kupitia migongo ya watu.”Winfrida
alikasirishwa sana na kitendo alichofanyiwa kaka yake.Alianza kubwabwaja maneno
yake kuntu utadhani aliyekuwa anamwambia alikuwa eneo lile.
“Sijajua ana lengo
gani hasa na mimi?”Denis alijisemea.
“Labda
anakutaka.”Brenda aliropoka huku akiwa anamtupia Vivian jicho la machale.
“Mbona unaniangalia
kwa wasiwasi hivyo wifi?”Vivian alimuuliza Brenda baada ya kumwona akimsorora
kwa jicho la pembeni.
“Usije ukanirukia
bure.Denis ni wako hachukuliwi na mtu yeyote.Kwahiyo Denis wewe umechukua
uamuzi gani juu ya suala hilo?Upo tayari kuhudumia mzigo usiokuhusu?”Baada ya
Denis kuulizwa swali hilo na mdogo wake,aliacha kula na kumtazama halafu
akatikisa kichwa kwa masikitiko.
“Kwa kuwa
nimeshajifunga mwenyewe kwa kusaini zile karatasi za polisi itabidi nimhudumie tu huyo binti mpaka
atakapopona.Halafu baad……….”
“Mmmh!mwenzangu una
hela za kuchezea.Kugongwa agongwe na mwingine halafu wewe ndiyo uhudumie!Kaka
yangu hapo umeliwa wala sikushauri.Tuna uwezo wa kulipeleka shauri hili
mahakamani na maamuzi mazuri yakatolewa.Wale ni polisi tu hawana
lolote.Tuliamua kukushauri usaini ili tu utoke katika mazingira yale lakini kwa
kweli sihafikiani na hilo suala hata punje.”Maneno ya Denis yalikatizwa na
mdomo wa Brenda aliyeanza kuongea kama cherehani.Alipingana kabisa na maelezo
ya kaka yake ya kutaka kumhudumia Shaimaa kama alivyosaini na kukubaliana na
masharti ya dhamana.
“Hata mimi mwenyewe
nipo upande wa Brenda.Haiwezekani utoe pesa zako kumhudumia mtu aliyekusingizia
kosa kama hilo.Msaada wako wa kumpeleka hospitali unatosha kabisa.Halafu hana
hata aibu,eti anajilizaliza mbele yetu kinafki.Anafikiri tungemchekea hivi
hivi!Hajui kama amekuingiza matatizoni au?Yule siyo mtu,hana ubinadamu hata
kidogo.Au unasemaje wifi?”
“Tupo pamoja.”Vivian
aliungana na wifi zake watarajiwa kumpinga Denis kutokana na maamuzi aliyotaka
kuyachukua.
“Acheni tu
nimhudumie,kwani itagharimu shilingi ngapi?Si itakuwa tu pesa ya mboga kwangu ndiyo imetumika!Naamua
kufanya hivyo ili nijue huyo binti ana nia gani hasa na mimi.Nafikiri
akishapona ataweza kuzungumza vizuri.”Siyo kwamba Denis hakuchukia ushenzi
aliofanyiwa na Shaimaa la hasha!Alichukia tena zaidi ya sana ikafika hatua
chuki ikajipandikiza ndani ya moyo wake juu ya binti huyo.Lakini alijitolea
kumhudumia ili awe karibu naye na mwishowe iwe rahisi kwa yeye kujua lengo lake
la kumsingizia hiyo kesi.
Alifikiri pengine huyo
binti anamfahamu na isingekuwa rahisi kiasi kile kuthubutu kumsingizia mtu
asiyemjua hata kidogo kesi kubwa namna ile.Pengine kama si hivyo,Denis alitaka
kujua ni kita gani kilichomsukuma kufanya hivyo.Majibu ya vyote alivyokuwa
anajiuliza hawezai kupata kwa mtu mwingine yeyote yule zaidi ya Shaimaa.
Ndiyo maana alikubali
kuibeba dhamana ile japokuwa mwanzoni aliipinga katakata,ili tu ajue mengi toka
kwa binti huyo.Kila mtu alijaribu kumpinga lakini Denis alishikilia maamuzi
yake na kuwaambia kuwa yeye ni mtu mzima anajua anachokifanya.
Baada ya kulumbana kwa
muda mrefu mwishowe wakaamua kusalimu amri.Denis alikubali kuubeba mzigo ule
akiamini kuwa Mungu atamlipa binti huyo kwani malipo ni hapa hapa duniani.Vile
vile aliamini pengine hilo ni jaribu la Mungu kwake ili amwone kama ana uwezo
wa kutoa msaada kiasi gani kwa wengine hata kama ni maadui zake.
Baada ya kumaliza kula
walikwenda mapokezi kwa lengo la kupata vyumba kwaajili ya kulala.Kwa bahati
mbaya waliambiwa vyumba vimejaa hivyo ikawalizimu kwenda kulala hoteli ya
jirani inayojulikana kwa jina la Nyinda hoteli.Dick na Dolan walichukua chumba
kimoja na Winfrida pamoja na Brenda nao wakachukua chumba kimoja.Vivian yeye
alikwenda kulala na Denis pale pale Dolphni hoteli.
Wakati huo huo Denis
alishazungumza na wazazi wake na kuwaambia kuwa ameshamalizana na polisi juu ya
sakata hilo.Aliwataka ndugu zake warejee Dar-es-salaam wakaendelee na shughuli
zao kwa kuwa yeye tayari yupo huru.
“Sasa Denis ulivyosema
kwamba sisi turudi nyumbani wakati hali yako bado haipo vizuri unamaanisha
nini?”Vivian alimuuliza Denis wakiwa kitandani huku akichezea kidevu cha
mwanaume huyo.
“Ha!ha!ha!ha!usiwe na
wasiwasi mpenzi wangu.Kwa sasa hivi nina hali nzuri tu.Hata ninyi wenyewe
mliniambia cha muhimu ni kuwa huru kwanza halafu mambo mengine ndiyo
yafuate.Nilichokuwa nakifuata Tanga bado sijakikamilisha.Sijatembelea ofisi
yangu hata moja kwahiyo kazi hiyo nataka nianze kuifanya kesho.Akina Dick
wameacha ofisi hazina msimamizi hata mmoja.Akina Brenda nao wana shughuli zao
na wewe pia hivyo hivyo.Sasa mtakaa na mimi hapa halafu kazi zenu mmwachie
nani?”Denis alizungumza na mchumba wake kwa sauti a upole.
“Basi wao warudi
halafu mimi nibaki.”Vivian alikuwa na kaugumu fulani ndani ya moyo
wake.Hakutaka kuamini kama mpenzi wake ataweza kugangaika mjini peke yake
ilihali bado hakuwa vizuri kiafya.
“Vivian,najua
unanipenda sana na kunijali kuliko maelezo.Lakini pamoja na yote hayo hatuwezi
kukaa pamaoja kila wakati halafu kazi zidorore.Huu utakuwa ni uzembe wa hali ya
juu sana.Nashukuru mmekuja kuniona na kunifanikiwa kunitoa ndani.Sasa
kinachoktakiwa ni kurudi makazini jamani!”
Denis alikuwa ni
mwanaume mchapa kazi kila dakika.Hakupenda vitu vidogo vidogo vimpotezee wakati
wake wa kuwajibika.Aliamini uwepo wa Vivian eneo lile litaathiri ufanisi wake
wa kazi kwani muda wote itakuwa ni mapenzi tu badala ya kufanya kilichompeleka
Tanga.Ndiyo maana aling’ang’ania watu warudi katika shughuli zao za uzalishaji
mali.
“Najua unanilazimisha
niondoke ili upate muda mzuri wa kumhudumia yule msichana.”Vivian alianza
kuyapeleka mawazo yake mbali kabisa.
“Unamaanisha nini
kusema hivyo?”Denis aliuliza kwa mshangao.
“Amna,kawaida tu.”Wivu
ulianza kutafuna Vivian akiamini kuwa Denis anafahamiana na Shaimaa hivyo
anamuondoa pale Tanga ili iwe rahisi kufanya mambo yake na msichana huyo
aliyekuwa hoi kitandani.
“Haya,kama umeshaanza
kuwaza vitu vingine ambavyo havipo,hiyo ni shauri yako.Unajipa presha za bure
bila sababu ya msingi.Tambua kuwa nakupenda sana kuliko mwanamke yeyote yule
ndani ya dunia hii.Wewe ndiyo ua la moyo wangu.Wewe ndiyo chakula cha moyo roho
yangu.Wewe ndiyo kioo changu,ndiyo muongozo wangu.Wewe ndiyo kila kitu katika
maisha yangu.Unapaswa kujiamini unapokuwa na mimi au unapokuwa mbali nami.”
“Haya baba
nimekusikia.”Vivian alimjibu Denis kisha akageukia ukutani na kulala.Denis
alibaki na mawazo juu ya hali ile iliyoionesha mchumba wake.
“Mmmh!huyu msichana
huwa ana wivu sana.Sijui ni kwanini huwa ajiamini katika mapenzi.Nakumbuka
kipindi kile kabla hajawafahamu akina Brenda alifikiri ni wasichana
wangu.Nashangaa tena sasa hivi ananiambia habari za yule msichana
mgonjwa!Kwahiyo anataka kuniambia na yule ni mwanamke wangu!Vivian punguza wivu
bwana,utakuja kujiua bure!”
Baada ya mawazo hayo
kuanza kupotea ndani ya kichwa cha Denis,taratibu usingizi ukaanza kumnyamelea
mdogo mdogo.Hakujua hata amelala saa ngapi lakini alikuja kushtuka baada ya
kudondokewa na matone ya maji baridi usoni.Alipofungua macho yake alimuona
Vivian akiwa na glasi ya maji mkononi.
*********
Itaendelea....Asante kwa ufuatiliaji wako wa hadithi hii.....Mungu akujalie afya njema.Nakutakia siku njema.
*******
Kwa maoni au ushauri napatikana kwa namba 0655089197/0766123623