STORY-PENZI LA MSHUMAA
MTUNZI-MZIRAY F.M.
SEHEMU YA 14
Ilipoishia sehemu ya 13
“Unaona sasa!We
unadhani Range Rover ni milioni ngapi? Sasa mtu kama wewe utasingiziwa kesi
gani?Utaambiwa umeiba kuku kama sisi?Kesi zenu ndiyo hizo za kugonga watu kwa
magari yenu,kupiga au kuua binadamu wenzenu.Sasa utasemaje umesingiziwa!” Kila mtuhumiwa ndani ya mahabusu ile
alimwandama Denis.
“Hana lolote huyo ni
mnafiki tu.Asingiziwe wapi!Ameamua kumpanda dada wa watu miguuni na Range lake.Bora ufungwe tu uwe
sawa na sisi.”
Sasa endelea......
“Kweli kabisa,bora
tufanane tu.Hawa huwa wanapeana ajira wenyewe.Utakuta ofisi yake wamejazana
ndugu chungu nzima.Nenda wewe sasa utaambiwa una vyetu vizuri lakini hakuna
ajira.”Denis alitengwa na kila mtu ndani ya lokapu ile.Wengi wao waliochukizwa
naye ni vijana wenye umri sawa na yeye na wachache sana waliomzidi.
Hawakupenda kijana
mwenye umri sawa na wao awe na mafanikio kiasi kile ilihali wao walikuwa
wanasota mitaani kutokana na ugumu wa maisha.Walitiwa mbaroni baada ya
kujiingiza kwenye makundi ya kihuni na kupora mali za watu.
Hawakutaka kujituma
katika kufanya kazi ili wajipatie kipato chao cha halali.Wanaisingizia serikali
kwa kutowapa ajira.Fursa za ajira mbona zipo chungu nzima sema vijana hawataki
kuzichangamkia.Pengine labda hakuna mazingira rafiki yatakayowasukuma kufanya
mambo ya maendelea.
Lakini kwa vijana
waliofanikiwa kama Denis wao waliwezaje?Si walikazana katika kufanya kazi kwa
bidii na mwisho wake matunda yanaonekana.Uvivu umewajaa vijana wengi wa nchi
hii ndiyo maana hawapati maendeleo.Hawataki kufanya kazi wanaishia kukaa
vijiweni na kupiga zogo tu.Wanabaki kuwapiga majungu wenzao
waliofanikiwa.Badala wajifunze toka kwa watu hao wanabaki kusema mali zao siyo
za halali.Mara yule alimtoa mama yake kafara ndiyo maana ni tajiri vile.Mara
huyu anafuga mandondocha ndani ya nyumba ndiyo maana ana mali chungu
nzima.Mtaendelea kusema mali za wenzenu tu lakini wao wanazidi kusonga mbele.
“Jamani inawezekana
kweli kasingiziwa tusimpinge moja kwa moja.”Mtuhumiwa mmoja alijitokeza na kuwa
upande wa Denis baada ya kuona wenzake wamemwandama sana kijana huyo.
“Haa!huyu anasema
nini?
“Mimi mwenyewe
namshangaa.”
“Wewe unamtetea huyu
unamjua?Unafikiri akitoka hapa atafanya mipango ya kukutoa humu ndani?Hizo ni
ndoto za alinacha kaka.”
“Huyu jamaa kagonga
kweli,wewe unatetea nini?”
“Nyie mmemuona
akimgonga huyo msichana?Kama amesingiziwa tu kisa kamuona jamaa ana hela ili
alipwe!Acheni hiyo,haya mambo ya kusingiziwa yapo kwa mtu yeyote bila kujali
kipato chake.Omba tu Mungu yasikukute maana utahisi umetengwa na dunia
nzima.”Yule jamaa kweli alidhamiria kumtetea Denis.
“Mbona unamtetea
sana?Huyu jamaa ndugu yako nini?”
“Siyo ndugu yangu ila
nawapa makavu.Acheni kumwandama mtu bila sababu ya msingi.Sisi wote tupo humu
ndani ni wa moja.Haina haja ya kuanza kuleta matabaka ilihali wote tupo kwenye
matatizo.”Kweli jamaa aliamua kumkingia Denis kifua.
“Kwani wewe
unasemaje?”
“Kuhusu nini?”
“Chochote kile.”Wale
watuhumiwa wengine baada ya kuona kuwa Denis kapata mtetezi wakaanzisha vurumai
ndani ya mahabusu.
Denis pamoja na yule
kijana aliyekuwa upande wake walipigwa sana mpaka wakaanza kuvuja damu.Askari
walipokwenda kutuliza ile vurumai hawakuchagua wa kumpa kisago.Walisambaza
mkong’oto mahabusu nzima bila kujali aliyeanzisha ugomvi wala aliyepigwa.
Masikini ya
Mungu,Denis aliumia vibaya mno maeneo ya usoni.Alipasuka paji la uso na upande
wa kushoto karibu na shavu.Alivuja damu uso mzima.Vile vile macho yake yote
mawili yalivimba sana baada ya kupigwa ngumi za usoni.Denis alijigaragara chini
kutokana na maumivu makali aliyokuwa anayasikia.Moyoni mwake alimlaani yule
msichana aliyemsingizia kesi isiyokuwa ya kwake.
Matatizo anayoyapata
yametokana na kauli ya Shaimaa kwamba Denis ndiyo kamgonga na kumvunja miguu
yake yote miwili wakati haikuwa hivyo.Denis alilia sana akawa haamini kama
kweli ipo siku ambayo angekuja kutumbukia kwenye shimo lenye miba mikali namna
hiyo.Hakujua atatoka lini ndani ya chumba kile kilichotawaliwa na giza totoro pamoja
na ufinyu wa hewa.
Alizoea kulala katika
chumba cha kisasa juu ya kitanda cha sita kwa sita.Lakini siku hiyo alijibanza
kwenye kona karibu na ndoo ya kinyesi iliyochanganyika na mikojo ya watuhumiwa
wenzake.Harufu iliyokuwa inatoka katika ndoo hiyo iliumiza sana pua yake.
Alijaribu kukabiliana
nayo lakini wapi!Alipiga chafya mfululizo kama beberu.Pia kulikuwa na joto kali
sana kutokana na mrundikano wa watu wengi katika chumba kidogo kama
kile.Watuhumiwa walipata shida mno lakini hawakuwa na namna nyingine ya
kuepukana na hatari hizo.Siku hiyo iliyoyoma bila Denis kufunga jicho lake
mpaka asubuhi.Kesho yake asubuhi majira ya saa tatu Denis alitolewa kule
mahabusu na kuingizwa chumba cha mapokezi.
“Kijana umeona maisha
ya humo ndani yalivyokuwa matamu?Kwa taarifa yako utakaa huko mwezi mzima kama
hautotupa maelezo ya kueleweka.”Yule askari mpelelezi aliutonesha moyo wa Denis
kwa maneno yale ya kejeli.
“Sasa afande unataka
nikupe maelezo gani mengine ya ziada?Mimi nimeshawaambia kuwa sjamgonga yule
binti.Kapimeni basi gari yangu muone kama kweli imefanya tukio hilo.”
“Gari tumeshaipima na
majibu ndiyo hayo.Wewe ndiyo uliyehusika na ajali hiyo.”
“Hivyo vipimo vyenu
siyo sahihi.”Deni alipingana na maelezo yale.
“Kijana chunga
sana.Kwahiyo mimi afisa mzima wa polisi ni muongo?Badala ya kuwa mpole ili
nikusaidie,wewe unaleta jeuri!Hii kesi ikienda mahakamani lazima ufungwe na
biashara zako zitaharibika.”Yule askari alianza kujikombakomba kwa Denis kwa
lengo la kumsaidia.Denis aliinua uso wake na kumtazama askari yule aliyekuwa
anajizungusha katika kiti chake.
“Kwahiyo wewe unataka
kunisaidiaje?”Denis aliuliza kwa upole.
“Hayo ndiyo maneno
sasa.Mimi sihitaji pesa yako hata kidogo.Nataka nikufanyie mpango wa dhamana
ili utoke humu ndani.”
“Ninachofahamu
mimi,dhamani ni haki yangu ya msingi.Sasa utasemaje kwamba wewe ndiyo wa
kunifanyia mpango wa dhamana!”Denis alijaribu kujitutumua.
“Sikiliza nikuambie
kijana,hapa duniani hakuna haki,haki ipo mbinguni.Sasa wewe neng’eneka kama
hujaozea jela na pesa zako.Wewe unadhani pesa zinaweza kufanya kazi kila
sehemu?Usiishi kwa kukariri utakufa.Shenzi kabisa!Haki haki,ungekuwa na haki
ungekuwepo hapa?Hebu fungua akili yako,siyo kila kabila linachezewa kijana.Hii
ndiyo Tanga waja leo waondoka leo.Tanga raha bwana.”Taarabu alizoimbiwa na yule
askari zilimshangaza sana Denis.Ilibidi awe mpole ili ajue jamaa anataka nini
toka kwake.
“Haya niambie
utanisaidiaje afande?”
“Nipe namba za simu za
ndugu yako yeyote yule nizungungumze naye ili afike hapa kituoni kwaajili ya
dhamana.Suala la masharti ya dhamana hiyo utayafahamu atakapofika huyo ndugu
yako.”Denis alitakiwa kutoa namba za
simu ili mawasiliano yafanyike aje kutolewa dhamana.
“Katika orodha ya
majina yaliyopo kwenye simu yangu kuna jina la Dick.Mpigie huyo mweleze yote
yaliyonisibu.Nadhani atakuja kunitolea hiyo dhamana.”Baada ya Denis kutoa
maelezo hayo alirudishwa lokapu na kutulia.Alishindwa kuelewa yule askari ana
lengo gani na yeye.Hata kama anataka kumsaidia lakini kwanini ampe maneno ya
kejeli kama yale.Hali hiyo ilizidi kumweka njia panda.
Mchana nao ukakatiza
bila kulishibisha tumbo la Denis kama ilivyokuwa asubuhi.Minyoo walipiga miayo
mfululizo ndani ya tumbo kuashiria kuwa walihitaji chochote kitu.Hata hivyo
Denis alishindwa kupambana na wazoefu wa mahabusu ile ili kupata chakula kidogo
kilichokuwa kinagawiwa.Ilipofika jioni majira ya saa 11 Denis alichukuliwa tena
na kupelekwa katika chumba cha mpelelezi.Alipofika ndani ya chumba hicho
hakuamini macho yake kwa kile alichokiona.
Mbele yake alisimama
Dickson na Dolan huku kwenye viti vya upande wa kushoto waliketi wadogo
zake,Brenda na Winfrida.Upande wa kulia aliketi mchumba wake pamoja na wazazi
wa Shaimaa.Walipomuona tu Denis katika hali ile kila mmoja alihamaki kivyake
kuonesha machungu aliyoyapata.
“Mamaaa!Mungu wangu!Denis!Denis
mchumba wangu nini kimekupata?Niambie Denis,niambie!”Vivian aliinuka na kwenda
kumkumbatia Denis kwa nguvu huku machozi yakimtoka.
“Jamani mmemfanya nini
kaka yetu Denis?Kwanini mmempiga?Masikini kaka Denis ameharibika uso mzima.”
“Uuuwi!Denis jamani
eeeh!Umefanya nini kaka yangu?”Brenda na Winfrida nao hawakubaki nyuma.Walianza
kuangua vilio baada ya kuyaona mabadiliko aliyokuwa nayo kaka yao.Dolan na Dick
aliugulia kimya kimya ndani kwa ndani.Si uanjua uwanaume ni kujikaza,basi
walijikikaza kisabuni lakini moyoni mwao walihuzunishwa sana na hali ya rafiki
yao ambaye ndiyo bosi mkuu katika kampuni yao ya mafuta.
“Shenzi!tulieni
wote!Hii siyo kliniki bali ni kituo cha polisi.Kuna kanuni na taratibu zake
hivyo zinapaswa kuheshimiwa na kila mtu.Nani kawaruhusu kulia?Binti nenda kakae
sehemu yako.Unajilizaliza nini hapa?”Vivian alimwachia Denis na kwenda kukaa
kwenye kiti chake baada ya kuchimbwa mkwara mzito na askari yule
mpelelezi.Kutokana na hali aliyokuwa nayo Denis,ilimhuzunisha kila mmoja aliyekuwa
ndani ya chumba kile.Hata wazazi wa Shaimaa walimwonea huruma kaka wa watu
kwasababu uso wake ulikuwa umeharibika sana.
Mavazi aliyokuwa
amevaa yalichanikachanika katika vurumai lililotokea ndani ya mahabusu.Kutokana
na utanashati aliozoeleka kuonekana nao,mtu akimtia machoni kwa muda ule lazima
adondoshe chozi bila kutarajia.Mawazo ya Denis yaliamua kutulia ili ajue
kitakachoendelea ni nini baada ya ndugu zake pamoja na wazazi wa Shaimaa kufika
pale kituoni.
“Hapa haina haja ya
kupoteza muda kwasababu tuna kazi kibao za kufanya.Kilichowaleta hapa ni suala
la zima la kumtolea dhamana huyu ndugu yenu ili aweze kutoka humu ndani.”Yule
askari alianza kuzungumza baada ya hali kuwa shwari.Lakini Brenda,Winfrida
pamoja na Vivian bado walikuwa wanalia chini kwa chini pindi walipokutanisha
macho yao na uso wa Denis.
“Lakini afande bado
hujatueleza Denis kafanya nini mpaka akaletwa hapa?”Dick aliamua kuyakatiza
kwanza maelezo ya askari yule ili wajue kosa la Denis hadi akatupwa
mahabusu.Alipompigia Dick simu majira ya saa tatu asubuhi,askari huyo
alimweleza tu kuwa Dick yupo kituo cha polisi Raskazoni tangu siku iliyopita
hivyo afike kwaajili ya kumtolea dhamana.
Baada ya Dick kupata
taarifa hiyo alikwenda kuwaeleza wazazi wa Denis ambapo alitumia gari lake dogo
kusafiri toka Dar-es-salaam mpaka Tanga akiwa na ndugu wa Denis,mchumba wake
pamoja na rafiki yao Dolan.Walifika Tanga saa 10 jioni ambapo waliulizia kituo
cha polisi Raskazoni mahali kilipo na baada ya kuelekezwa wlaikwenda moja kwa
moja hadi kutuoni hapo kumwona Denis.
Hivyo basi,tangu
walipotoka Dar-es-salaam hawakujua Denis kafanya kosa gani mpaka akaingia
katika matatizo makubwa kiasi kile.Ndiyo maana Dick akataka kujua kosa lake
kabla ya masuala ya dhamana hayajafuata.
“Mnawaona hawa wazee
hapa mbele yenu?”Afande alipouliza swali hilo kila mtu alihamishia macho kwa
wazazi wa Shaimaa.
“Ndiyo tunawaona.”Wote
walijibu kwa pamoja.
********
Itaendelea........Tunaomba radhi kwa kutorusha simulizi hii kwa majuma kadhaa....Hii ilisababishwa na kuharibika kwa kompyuta iliyokuwa inatumika kupostia hadithi.Sasa hivi tumerudi kwa kasi na simulizi itaendelea kama kawaida.Nawatakia siku njema na Mungu awabariki sana.
******
Kwa maoni au ushauri napatikana kwa namba 0655089197/0766123623