STORY-PENZI LA MSHUMAA
MTUNZI-MZIRAY F.M.
SEHEMU YA 15
Ilipoishia sehemu ya 14
Hivyo basi,tangu
walipotoka Dar-es-salaam hawakujua Denis kafanya kosa gani mpaka akaingia
katika matatizo makubwa kiasi kile.Ndiyo maana Dick akataka kujua kosa lake
kabla ya masuala ya dhamana hayajafuata.
“Mnawaona hawa wazee
hapa mbele yenu?”Afande alipouliza swali hilo kila mtu alihamishia macho kwa
wazazi wa Shaimaa.
“Ndiyo tunawaona.”Wote
walijibu kwa pmaoja.
Sasa endelea..........
“Basi hapo walipo wana
huzuni tele baada ya huyu kinyago kumgonga mtoto wao na kumvunja miguu yote.Kwa
bahati nzuri alipata kidogo moyo wa huruma na kumbeba huyo binti hadi
hospitalini hapo Bombo.Lakini cha kushangaza baada ya kumfikisha hospitali
akataka kutoroka na kumsusia msichana wa watu pale Bombo ilihali akiwa katika
hali mbaya sana.Basi madaktari kuona vile wakatupigia simu mara moja tufika
pale na kumdhibiti.Kama huyo binti atafariki dunia huyu lazima apelekwe
mahakamani kwa kesi ya mauaji.”Afande alimaliza kuwaeleza kosa la bandia
alilolifanya Denis.Kila mtu aliinamisha kichwa chini kwa masikitiko.
“Sasa ndiyo mumpige kiasi
hicho?”Vivian aliropoka baada ya uvumilivu kumshinda.
“Unasemaje we
binti?Hebu ngoja,nadhani hujatujua vizuri.Hello!over,over!naomba askari wanne
hapo.Haraka sana wafike ofisini kwangu.”Yule afande alikasirishwa sana kwa
kitendo cha Vivian kumkaripia kwa sauti ya ukali.
“Hivi we binti una
akili timamu?Unasema huyo kapigwa!Umemwona mwanangu alivyosagika miguu yake?Au
unadhani sisi wazazi tumelifurahia hilo suala?Kwahiyo ninyi ndiyo mna uchungu
sana kuliko huyo mwanetu aliyepewa ulemavu wa kudumu!Sisi ni wazazi wake lazima
tuumie kushinda hata ninyi.Mtoto anauma ati!”Mama yake Shaimaa alimcharukia
Vivian baada ya kuonesha waziwazi kuumizwa na kitendo alichofanyiwa mchumba
wake.
“Mama usiwe na
wasiwasi huyu nitamshikisha adabu sasa hivi.”Yule askari alimtuliza Bi Zena kwa
kumwambia kuwa atamshughulikia Vivian yeye mwenyewe.Dakika moja mbele mlango wa
kile chumba ukafunguliwa na askari wanne wakaingia wakiwa na virungu
mkononi.Deni alipoona vile alianza kumwombea msamaha mchumba wake.Aliijua
vizuri kazi ya vile virungu maana kibano alichokipata siku iliyopita
hakielezeki.
“Afande tafadhali
naomba umsamehe huyo binti.Hilo siyo kosa lake ameteleza tu afande.Naomba
umsamehe ama kama vipi niadhibu mimi badala yake.”
“Hapana,huyu hawezi
kutupangia kazi.Hili ni jeshi la polisi siyo danguro.Kama umezoea kuwa bania
pua hao unaowauzia uchi siyo hapa,ni huko huko.Vijana!”Yule askari aliita kwa
sauti ya ukali.
“Naam afande.”
“Nataka huyu binti
arudi hapa akiwa hatamaniki.”
“Sawa afande.”
“Afande jamani
nakuomba umsamehe tu bure.Niadhibu mimi badala yake.Tadhali afande nipo chini
ya miguu yako.”Denis alidiriki kudondosha machozi akimwombea Vivian
msamaha.Kweli polisi fanya nao masihara wanapokuwa mtaani.Ukishaingia kwenye
18 zao inabidi uwe mpole kama maji
mtungini la sivyo utaonja joto ya jiwe.
Hawa jamaa wapinge kwa
kutumia sheria lakini siyo kuwaropokea ovyo.Hakika watakutengenezea zengwe
ambalo litakuingiza matatizoni mzima mzima.Hata kama utakuja kufanikiwa
kulitatua zengwe hilo lakini tayari watakuwa wamekupotezea muda wako na
shughuli zako kudorora.Hilo ndilo lililotaka kumkuta Vivian baada ya kuwa
mropokaji ndani ya kituo cha polisi.Ni bora uwe mpole kwanza halafu kama
utahisi kuwa umeonewa una haki ya kikatiba inayokuruhusu kuwafungulia mashtaka
mahakamani.
Malalamiko ya Denis
yalimfanya yule afande aligeze kamba. “Haya hebu mwacheni.Nyama wewe!Siku
nyingine usirudie kuleta upumbavu wako kwenye kituo cha polisi.Shenzi
kabisa,Malaya wa kale wewe!”Denis aliachia tabasamu hafifu baada ya mchumba
wake kusamehewa.
“Afande nini
kinaendelea hapa?Sisi tunataka tukamtazame mwanetu.”Mzee Kambi aliuliza
kinachofuata kwani walikuwa na safari ya kwenda Bombo hospitali kumjulia hali
binti yao Shaimaa.
“Tulia mzee wangu
tuyamalize sasa hivi.Najua mna uchungu mno juu ya hali ya mtoto wenu.Sasa ni
hivi,Dick,si mmekuja kumwombea Denis dhamana?”
“Ndiyo afande.”Dick
alijibu kwa unyenyekevu.
“Dhamana tutakupatia
bila gharama zozote zile kwasababu ni haki ya mtuhumiwa kupata dhamana.Lakini
kutokana na kosa alilolifanya na hali aliyokuwa nayo binti wa hawa wazee kule
hospitalini,dhamana hiyo itakuwa na masharti kadhaaa.Je mpo tayari?”Afande
aliwauliza akina Dickson.
“Ndiyo tupo
tayari.”Dick alijibu kwa niaba ya wenzake.Denis akiwa na pingu zake mkononi
aliinua uso wake sambamba na kuyafungua masikio yake ili asikie hayo masharti
ya dhamana.Yule askari aliwaangalia wazazi wa Shaimaa kisha akahamishia macho
yake kwa ndugu wa Denis.Aliachia tabasamu kisha akalisawazisha koo lake na
kuanza kuzungumza.
“Kutokana na kosa
alilolifanya bwana mdogo Denis hapa,itabidi awajibike kwa kulipa gharama zote
za matibabu ya huyo binti aliyemvunja miguu.Gharama hizo ni za kuanzia jana
alipofanya tukio hilo mpaka pale atakapopona.Wakati huo uchunguzi bado
ukiendelea kufanyika na kama ikigundulika kuwa Denis hakuhusika na ajali hiyo
basi anayo haki ya kufungua kesi ya madai ya fidia mahakamani na atalipwa
gharama zake zote alizotoa hospitalini.Sambamba na hilo kila tutakapomhitaji
basi afike hapa kituoni kwa wakati.Hayo maelezo niliyowapa yapo kwenye hizi
karatasi na kama mkikubaliana nayo mtatia sahihi zenu hapo chini.”
Dick alichukua
karatasi moja yenye yale masharti ya dhamana na kuanza kuisoma.Denis naye
alipewa ya kwake na baada ya kuisoma aliinua uso wake na kumtazama Dick ambaye
naye alikuwa anamwangalia.Wazazi wa Shaimaa baada ya kupitisha macho juu ya
karatasi zile walizihamishia kwa akina Brenda ambao nao walisoma na
kuridhika.Kilichobaki ilikuwa ni maamuzi tu ya Denis kama atakubaliana na
masharti yale ama la!
Moyo wa Denis
ulionesha ugumu kidogo juu ya suala lile.Japokuwa alikuwa katika mazingira
magumu lakini hakutaka kutwishwa mzigo mkubwa kiasi kile.Siyo kwamba hakuwa na
fedha la hasha!Aliamini kuwa anaonewa
kwa kupewa majukumu ambayo hayastahili.
Hivyo basi,Denis
alitikisa kichwa kuashiria kutokubaliana na masharti yale.Kila mtu alimshangaa
kwani hali aliyokuwa nayo ni mbaya sana na asingestahili kuendelea kukaa ndani.
“Denis,kwanini hutaki kukubaliana na hili?Eti afande,tukishasaini hapa si
anatoka leo leo.”Dolan ndiyo alishangaa zaidi ya wengine.Hakutarajia kama Denis
angekuwa tayari kuendelea kukaa mahabusu.
“Denis,kaka Denis hili
suala mbona ni dogo sana kwako!Inamaana utashindwa kumhudumia huyo msichana?Una
pesa kiasi gani kaka?Tusaini tu ili uwe huru kwanza,mambo mengine
tutayashughulikia ukiwa nje.”Winfrida naye alihamaki baada ya Denis kupingana
nao.Brenda na Vivian waliamua kukaa kimya huku wakimwangalia Denis kwa
masikitiko.
“Jamani mimi
nimeshawaambia kuwa sijamgonga huyo binti.Kwanini nikubali kubeba mzigo ambao
siyo wa kwangu!Acheni tu niendelee kukaa humu ndani mpaka siku watakayonipeleka
mahakamani.Hiki ni kituo tu cha polisi hawana haki ya kunihukumu kwa lolote
lile.Eti nimuhudumie huyo msichana!kwani hawa ni mahakimu?Ushahidi wa kwamba
mimi ndiyo nimemgonga upo wapi?Kwa hili siwezi kukubaliana nalo.”
“Denis come on my
brother.Sikiliza nikuambie rafiki yangu,tufanye kwanza mpango wa kutoka hapa
halafu tutalifuatilia hili suala kwa kina.Chamsingi uwe kwanza huru hayo
mengine baadae.”Dick naye hakusita kumsihi rafiki yake akubaliane na yale
masharti ili atoke eneo lile.Uzalendo ulimshinda tena Vivian baada ya kumwona
mchumba wake akiendelea kung’ang’ania kubaki mahabusu.Aliinuka na kupiga hatua
kadhaa mpaka alipomfikia Denis.Alipiga magoti mbele yake na kumkumbatia huku
akimwaga machozi kwa uchungu.
“Denis naomba tu
ukubaliane na hayo masharti ili utoke hapa.Tazama jinsi ulivyokuwa katika hali
mbaya namna hiyo.Umelala tu usiku wa jana,je,ukikaa wiki nzima
itakuaje?Unanihuzunisha mno mimi mpenzi wako kila ninapokuona katika hali
hiyo.Si mimi tu,tazama ndugu zako Brenda na Winfrida wanavyokulilia.Waangalie
marafiki zako Dick na Dolan wanavyohuzunika kwaajili yako.Wazazi wako ndiyo
hawana hali kabisa,wapo hoi bin-taaban.Waliposikia habari hizi juu ya matatizo
yaliyokupata walilia sana.Sasa tutakwenda kuwaambia nini tukirudi mikono
mitupu?Tafadhali nakusihi kubaliana nao,hayo mengine tutafuatilia baadae.”
Ushawishi wa mpenzi
huwa na nguvu sana kuliko wa mtu mwingine yeyote yule.Maneno yaliyotoka katika
kinywa cha Vivian yalimshambulia Denis na kulainisha moyo wake ambapo aliamua
kukubaliana na yale masharti ya dhamana ili aweze kutoka.Baada ya kutia sahihi
yake wazazi wa Shaimaa nao walisaini halafu wakakabidhi kwa mashahidi ambao ni
Dick,Dolan,Brenda,Winfrida pamoja na
Vivian.Vile vile hata wale askari wengine waliokuwepo mule ndani nao walisaini.
Baada ya zoezi hilo
kukamilika,Denis alikabidhiwa baadhi ya vitu vyake na vingine aliambiwa aviache
pale kama dhamana.Waling’ang’ania vitambulisho vya kazi pamoja na leseni
yake.Vile vile Dick naye aliacha kitambulisho chake kama shahidi wa
dhamana.Denis alitolewa nje na kukabidhiwa gari lake ambapo kila mtu alishangaa
mno.
“Haaa!kaka Denis ndiyo
umenunua hii gari!Duuh!ni noma.”
“Jamani mume
wangu,hongera.Tabasamu basi kidogo mpenzi wangu!”
“Denis si utabasamu
jamani baby anakuomba.Au unatuonea aibu dada zako?”Brenda aliamua kuvunja
ukimya aliokuwa nao kwa muda mrefu.Denis aliachia tabasamu nono na kuwakumbatia
wote waliokuja kumtolea dhamana.Kila mmoja alimpa pole kwa yale
yaliyomkumba.Baada ya hapo Denis alimkabidhi Dick funguo yake ya gari na
kumwambia yeye ndiyo awe dereva.Dick naye alitoa funguo ya gari alilokuja nalo
toka Dar-es-salaam na kumrushia Brenda.
Walipomalizana na wale
askari,waliwapakia wazazi wa Shaimaa na kuelekea Bombo hospitali.Walipofika
ndani ya hospitali hiyo Denis alielekea ndani ya chumba cha daktari.Kwa bahati
nzuri hakumkuta yule dokta aliyemchoma kwa polisi siku aliyompeleka Shaimaa
pale hospitali.Alifanyiwa mattibabu ya uso wake sambamba na kupewa dawa za
kupunguza maumivu ya mwili.Baada ya kutoka kwa dokta hakumkuta mtu mwingine
yeyote kwenye benchi la kupumzikia zaidi ya mchumba wake,Vivian.Walitazamana
kwa sekunde kadhaa kabla ya kukumbatiana kwa nguvu.
Kila mmoja alivuta
hisia za mapenzi kwa mwenzake.Walibembelezana huku wakipapasana migongoni mpaka
walipotosheka.Baada ya kuachinana Denis aliuliza watu wengine wapo wapi ndipo
Vivian alipomvuta mkono na kmpeleka kwenye hodi aliyolazwa Shaimaa.
Alipoingia ndani ya
chumba hicho alikuta kitanda alicholala msichana huyo kikiwa kimezungukwa na
wazazi wake pamoja na akina Dick,Dolan na wadogo zake.Denis alipofika tu kila
mmoja aligeuka na kumtazama kwa huruma.Alikuwa anachechemea kwa mbali kutokana
na kupigwa kwa virungu vya polisi maeneo ya magoti.
Denis alipomtazama
Shaimaa hasira zilimkaba akashindwa kuzungumza.Badala yake alimwaga machozi
kuyapoza machungu aliyokuwa nayo.Alijiuliza ni kwanini msichana huyo aliamua
kumsingizia ajali ambayo hakuhusika nayo.Alishindwa kuelewa ni kipi hasa
kilichomfanya Shaimaa kumsukumia yeye mzigo usiokuwa wa kwake.Kutokana na
hilo,moyo wake ulimea chuki yenye kutu juu ya msichana yule.
Hakutaka kuonesha
waziwazi kuwa anamchukia Shaimaa.Badala yake aliamua kujikaza na kujipa muda
ili ajue lengo hasa la msichana huyo kumfanyia udhalilishaji ule.Hakika Denis
alishadhalilika sana mbele ya madaktari na manesi wa pale Bombo.Vile vile
alipopelekwa polisi alidhalilishwa na askari wa kituo kile pamoja na mahabusu
wenzake.Kila alipokumbuka matukio hayo aliumia sana moyoni.
“Basi Denis usilie
mpenzi wangu.Haya mambo tutayamaliza tukishatoka hapa.Tutazungumza kwa kirefu
na wazazi wa huyu binti tujue tunamalizana vipi nao ili turudi
Dar-es-salaam.”Vivian alimfuta Denis machozi na kumwambia akaze moyo yeye ni
mtoto wa kiume.Alimshika mkono na kusogea naye karibu na kitanda cha Shaimaa.
*********
Itaendelea.....Nashukuru kwa ufuatiliaji wako wa hadithi hii.Nakutakia siku njema na Mungu akujalie afya tele ili uweze kutimiza majukumu yako ya kila siku.
*********
Kwa maoni au ushauri napatikana kwa namba 0655089197/0766123623